Levante yaduwaza miamba Atletico Madrid ligini

Levante yaduwaza miamba Atletico Madrid ligini

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Atletico Madrid, kuhifadhi ufalme wa kipute hicho msimu huu yalididimizwa zaidi na Levante waliowapokeza kichapo cha 1-0 mnamo Jumatano usiku ugani Wanda Metropolitano.

Gonzalo Melero alifungia Levante bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo. Angel Correa alidhani alikuwa amesawazishia Madrid mwishoni mwa kipindi cha pili ila bao hilo likafutiliwa mbali kwa madai kwamba mpira ulijazwa kimiani baada ya mchezaji wa Levante kukabiliwa visivyo.

Levante nusura wafunge bao la pili kupitia Mickael Malsa ila kombora lake likabusu mwamba wa goli. Kichapo hicho kilisaza Atletico katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la La Liga baada ya kupoteza mchuano wa sita kati ya 10 iliyopita.

Sasa wana alama 39 sawa na nambari nne Barcelona ambao wana mechi moja zaidi ya kutandaza ili kufikia idadi ya michuano 24 ambayo imesakatwa na Atletico. Real Madrid wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 54, nne kuliko nambari mbili Sevilla na 11 zaidi kuliko Real Betis wanaofunga mduara wa tatu-bora.

Chini ya kocha Diego Simeone, Atletico kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Osasuna mnamo Februari 19, 2022 kabla ya kualika Manchester United kwa gozi la hatua ya 16-bora kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Februari 23, 2022.

You can share this post!

Maseneta wagonga mwamba

Bayern na Salzburg nguvu sawa katika mkondo wa kwanza wa...

T L