Michezo

Lewandowski afikisha mabao 250 kwenye Bundesliga

December 17th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ROBERT Lewandowski alifunga mabao mawili katika ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Bayern Munich dhidi ya VfL Wolfsburg katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Jumatano.

Bayern walitoka chini kwa bao moja na kukomesha rekodi ya awali ya kutoshindwa kwa Wolfsburg katika kampeni za Bundesliga.

Ufanisi huo ulimwezesha fowadi huyo raia wa Poland kupitisha idadi ya mabao 250 kwenye Bundesliga.

Lewandowski, 32, sasa ndiye mchezaji wa tatu wa Bayern kuwahi kufikia hatua hiyo baada ya Gerd Muller na Klaus Fischer.

Maximilian Philipp aliwaweka Wolfsburg kifua mbele katika dakika ya tano kabla ya Lewandowski kufunga bao lake la 250 mwishoni mwa kipindi cha kwanza kisha akapachika jingine wavuni, la 251, baada ya kumwacha hoi kipa Koen Casteels kunako dakika ya 50.

Bao la pili lililofungwa na Lewandowski katika mchuano huo lilikuwa lake la 18 hadi kufikia sasa katika mashindano yote ya msimu huu wa 2020-21. Nyota huyo kwa sasa amefunga jumla ya mabao 73 kutokana na mechi 64 tangu mwanzoni mwa msimu wa 2019-20.

Alama tatu ambazo Bayern walijizolea dhidi ya Wolfsburg zinawaweka katika nafasi ya pili kwa alama 27 sawa na nambari tatu RB Leipzig.

Bayer Leverkusen wanaselelea uongozini kwa alama 29.