Michezo

Lewandowski afunga mawili na kubeba Bayern Munich hadi kileleni mwa jedwali la Bundesliga

December 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

NYOTA Robert Lewandowski alifunga mabao mawili na kusaidia Bayern Munich kutoka nyuma na kuwacharaza Bayer Leverkusen 2-1 katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Jumamosi.

Ushindi huo wa Bayern uliwapaisha hadi kileleni mwa jedwali kwa alama 30, mbili zaidi kuliko Leverkusen na RB Leipzig wanaoshikilia nafasi za pili na tatu mtawalia.

Patrick Schick aliwafungulia Leverkusen ukurasa wa mabao katika dakika ya 14 kabla ya Lewandowski aliyetawazwa na FIFA kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2020 kusawazishia Bayern mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Mshambuliaji huyo ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland, alifunga bao la pili na la ushindi kwa upande wa Bayern katika dakika za mwisho za kipindi cha majeruhi.

Chipukizi raia wa Uingereza, Jamal Musiala, 21, anayechezea Bayern, alishuhudia kombora lake likigonga mwamba wa goli la Leverkusen katika dakika ya 79.

Mabao mawili yalifungwa na Lewandowski, 32, sasa yanampa uhakika wa kufunga kampeni za mwaka wa 2020 akijivunia mabao 47 kutokana na mechi 44.