Michezo

Lewandowski aiongoza Bayern Munich kuizamisha Fortuna Dusseldorf

May 31st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ROBERT Lewandowski alifunga mabao mawili na kusaidia Bayern Munich kusajili ushindi mnono wa 5-0 dhidi ya Fortuna Dusseldorf katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Ushindi wa Bayern ambao kwa sasa wana jumla ya alama 67 kutokana na mechi 29, uliwawezesha kufungua pengo la alama 10 kileleni mwa jedwali na kutia mkono mmoja kwenye ufalme wa taji la Bundesliga kwa msimu wa nane mfululizo.

Bayern walijivunia matokeo ya 3-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza kupitia mabao ya Benjamin Pavard na Lewandowski waliotikisa nyavu baada ya Mathias Jorgensen kujifunga na kuwafungulia wenyeji wao karamu ya magoli.

Bao la 43 la Lewandowski katika michuano yote ya hadi kufikia sasa msimu huu lilifanya mambo kuwa 4-0 kunako dakika ya 50 kabla ya tineja Alphonso Davies kufunga la tano sekunde chache baadaye.

Ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba Bayern hawapo radhi kuachilia ubingwa wa msimu huu ambao umeratibiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa Juni 2020.

Huenda Borussia Dortmund wakapunguza pengo la alama kati yao na Bayern hadi kufikia saba zikiwa zimesalia mechi tano zaidi za kusakatwa muhula huu iwapo watakwaruza kesho limbukeni Paderborn ugenini.

Ushindi wa Bayern ulikuwa wao wa nne mfululizo tangu kivumbi cha Bundesliga kirejelewe mnamo Mei 16 baada ya kusimamishwa mwanzoni mwa Machi kutokana na janga la corona.

Miamba hao wa soka ya Ujerumani wanajivunia jumla ya mabao 13 na kufungwa mawili pekee kutokana na mechi hizo.

Chini ya mkufunzi Uwe Rosler, Dusseldorf walishuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo wakijivunia rekodi ya kutoshindwa katika msururu wa michuano sita iliyotangulia.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Jumamosi):

Bayern 5-0 Dusseldorf

Mainz 0-1 Hoffenheim

Schalke 0-1 Werder Bremen

Hertha Berlin 2-0 Augsburg

Wolfsburg 1-2 Frankfurt