Michezo

Lewandowski apiga mawili ndani

June 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

ROBERT Lewandowski alifungia Bayern Munich mabao mawili naye chipukizi Braut Haaland akafungia Borussia Dortmund magoli mawili katika mechi ambazo zilishuhudia klabu hizo mbili za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) zikisajili ushindi ikisalia mechi moja zaidi kwa kampeni za msimu huu kutamatika rasmi.

Bayern ambao walishuka dimbani kwa minajili ya mchuano wao wakiwa tayari wamejinyakulia ubingwa wa Bundesliga msimu huu katika mechi ya awali iliyowakutanisha na Werder Bremen, waliwapepeta Freiburg 3-1 uwanjani Allianz Arena.

Dortmund kwa upande wao walijipa uhakika wa kukamilisha kampeni za msimu huu katika nafasi ya pili kwa kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya RB Leipzig ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 63, sita nyuma ya Dortmund. Bayern wanaselelea kileleni kwa pointi 79.

Bremen waliopokezwa kichapo cha 3-1 na Mainz wananing’inia pembamba mkiani mwa jedwali kwa alama 28, nane zaidi kuliko limbukeni Paderborn ambao tayari wameshushwa ngazi.

Bremen ambao ni mabingwa mara nne wa taji la Bundesliga kwa sasa wana ulazima wa kupiga Cologne katika mchuano wao wa mwisho wa jedwali na kutarajia kwamba Fortuna Dusseldorf watapoteza dhidi ya Union Berlin ugenini.

Iwapo hilo litatokea, basi watajikatia tiketi ya kushiriki mchujo dhidi ya kikosi kitakachoibuka cha tatu kwenye msimamo wa jedwali la Bundesliga 2 ili kubaini kikosi cha tatu kitakachoshuka daraja kwenye Bundesliga na kile cha tatu kitakachopanda ngazi kuwania ubingwa wa ligi hiyo kuu msimu ujao wa 2020-21.

Lewandowski kwa sasa anajivunia jumla ya mabao 33 katika kipute cha Bundesliga msimu huu na anashikilia rekodi ya kuwa sogora wa kigeni katika Bundesliga kuwahi kupachika wavuni idadi kubwa zaidi ya mabao katika historia ya kipute hicho.

Kufikia sasa, nahodha huyo wa timu ya taifa ya Poland, amewafungia Bayern jumla ya magoli 47 katika mapambano yote ya msimu huu.

Kwa upande wake, tineja mzawa wa Norway, Haaland, alifikisha mabao 13 kapuni mwake akiwa ndani ya jezi za Dortmund msimu huu. Ina maana kwamba chipukizi huyo wa zamani wa RB Salzburg nchini Austria, amekuwa akicheka na nyavu za wapinzani wao kwenye Bundesliga kila baada ya dakika 75.

Katika mechi za raundi ya mwisho ya kipute cha Bundesliga msimu huu mnamo Juni 27, Bayern watakuwa wageni wa VfL Wolfsburg huku Dortmund wakiwaalika Hoffenheim.

Wolfsburg na Hoffenheim watakuwa katika ulazima wa kuibuka na ushindi kila mmoja ili kujipa tiketi ya kujiunga na Borussia Monchengladbach na Bayer Leverkusen ambao tayari wamefuzu kushiriki kivumbi cha Europa League msimu ujao.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Juni 20):

Bayern 3-1 Freiburg

Leipzig 0-2 Dortmund

Cologne 1-1 Frankfurt

Mainz 3-1 Bremen

Schalke 1-4 Wolfsburg

Dusseldorf 1-1 Augsburg

Hertha Berlin 2-0 Leverkusen

Paderborn 1-3 M’gladbach

Hoffenheim 4-0 Union Berlin