Michezo

Ligi kuu ya hoki kurejelewa mwezi mmoja baada ya Covid-19 kudhibitiwa

May 16th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MIPANGO ya Shirikisho la Hoki la Kenya (KHU) ya kurejelea kampeni za Ligi Kuu mwezi mmoja baada ya janga la virusi vya corona kudhibitiwa vilivyo imepokelewa vyema na mvamizi matata wa Butali Warriors, Calvins Kanu.

Azimio la kipute cha hoki kuanza upya siku 30 baada ya corona kudhibitiwa limedokezwa na Katibu Mkuu wa KHU, Wycliffe Ongori.

Kwa mujibu wa Kanu, muda huo utatosha vikosi vya Ligi Kuu kujifua vilivyo kwa muhula mpya kwa kuwa wachezaji wengu kwa sasa wanajifanyia mazoezi na hivyo itakuwa rahisi zaidi kurejea katika ubora wa fomu watakaporejea kambini kwa mazoezi mazito.

Kanu ambaye alifunga jumla ya mabao sita katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Butali, anatazamia kuwa ushindani utashuka pakubwa ligini katika hatua za mwanzo kutokana na likizo ndefu ambayo kwa sasa inashuhudiwa kabla ya viwango kuimarika zaidi kadri ya mpito wa muda.

“Kwa kuwa tumekuwa tukifanya mazoezi nyumbani, kipindi cha mwezi mmoja kitatosha kujirejesha katika ubora wa fomu na kuanza kunogesha michuano ya Ligi Kuu. Tayari tumepoteza muda mrefu kutokana na corona lakini mambo yatakuwa shwari,” akasema nyota huyo wa zamani wa klabu ya Kenya Police.

Kanu analenga kupata fursa ya kuwajibishwa mara kwa mara katika kikosi cha kwanza. Hata hivyo, atalazimika kutoana jasho na sajili mpya Festus Onyango aliyetokea Strathmore kupiga jeki viungo Amos Barkibir na George Mutira.

“Kubwa zaidi katika maazimio yangu ni kujituma kadri ya uwezo na kufunga magoli mengi iwezekanavyo. Ushindani ni mkali kikosini na italazimu kila mmoja kutia bidii mazoezini ili kuridhisha benchi ya kiufundi,” akasema.

Hadi kusitishwa kwa kampeni zote za msimu huu, Ligi Kuu ya Hoki kwa upande wa wanaume ilikuwa haijaanza lakini ligi za wanawake katika kategoria zote zilikuwa zikiendelea.