Michezo

LIgi kuu ya Ufaransa haitarejelewa msimu huu

April 29th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

LIGI Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) na Ligi ya Daraja la Kwanza nchini humo hazitarejelewa msimu huu baada ya serikali ya Ufaransa kufutilia mbali shughuli zote za michezo, hata kama zingeendeshwa katika viwanja vitupu, hadi Septemba 2020.

Waziri Mkuu wa Ufaransa, Edouard Philippe, amesema kwamba msimu huu wa 2019-20 umetamatika rasmi na atatangaza utaratibu mwepesi utakaoongoza mchakato wa kurejesha ukawaida wa maisha kuanzia Mei 11, 2020.

Awali, yalikuwa matarajio ya Shirikisho la Soka la Ufaransa (LFP) kuanza upya kampeni za msimu mnamo Juni 17 na kutamatisha vipute vyote vya kandanda nchini humo kufikia Julai 25, 2020.

Shughuli zote za soka nchini Ufaransa ziliahirishwa mnamo Machi 13, 2020.

Bado haijabainika iwapo LFP litafutilia mbali msimu huu mzima na kuamua kwamba hakuna mshindi wala kikosi kitakachopandishwa daraja au kushushwa ngazi.

Ingawa hivyo, magazeti mengi nchini Ufaransa yameshikilia kwamba huenda LFP ikatumia matokeo ya hadi kufikia wakati ambapo soka ya Ufaransa ilisitishwa kutawaza bingwa wa Ligue 1, kushusha baadhi ya vikosi kwenye kipute hicho na kupandisha ngazi klabu nyinginezo kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza.

Kufikia sasa, mabingwa watetezi Paris Saint-Germain (PSG) wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 12 zaidi kuliko Olympique Marseille ambao wanashikilia nafasi ya pili.

Hadi kivumbi cha Ligue 1 kilipositishwa, zilikuwa zimesalia mechi 10 zaidi kwa kampeni za msimu huu kutamatika rasmi.

Toulouse wanakokota nanga mkiani mwa jedwali kwa alama 17 nje ya mduara wa hatari na pengo la pointi 10 linatamalaki kati yao na Amiens ambao wanashikilia nafasi ya 19 kwenye orodha hiyo ya vikosi 20. Nimes wanakamata nafasi ya 18 kwa alama 27, tatu nyuma ya St Etienne.

Kwa upande wake, Nasser Al-Khelaifi ambaye ni Mwenyekiti wa PSG alisema: “Tunaheshimi maamuzi ambayo yametolewa na serikali ya Ufaransa. Kwa sasa tunapanga kuelekeza makini yote kwa kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) wakati wowote kitakaporejelewa na mahali popote kitakapoamuliwa kufanyika.”

“Iwapo itaamuliwa kwamba itakuwa hatari kwa kipute hicho kupigiwa nchini Ufaransa, jinsi dalili zote zinavyoashiria, tutakuwa radhi kusafiri popote patakapopendekezwa bora tu pawe mahali salama kwa wachezaji, makocha na maafisa wa PSG,” akaongeza.

Vikosi vitano vya kwanza kwenye jedwali la Ligue 2 vinatenganishwa na alama nne pekee huku klabu za Lorient na Lens zikishikilia kwa sasa nafasi za kupandishwa ngazi moja kwa moja hadi Ligue 1 muhula ujao.

Mnamo Aprili 10, vinara wa LFP walikutana na kupiga kura za kuamua kwamba kivumbi cha Ligue 1 kingalirejelewa mnamo Juni 17.

Ligi Kuu zote za bara Ulaya zina hadi Mei 25 kuwaeleza vinara wa Uefa iwapo zinataka kukamilisha misimu yao au kuifutilia mbali.

Javier Tebas ambaye ni Rais wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) amesema: “Nashangazwa na tangazo la Ufaransa. Sielewi kabisa jinsi ambavyo itakuwa hatari kuchezea soka ndani ya viwanja vitupu wakati ambapo juhudi zote zinaelekezwa kuhakikisha kwamba kuna usalama mkubwa wa wachezaji, maafisa wa timu, makocha, marefa na wadau wote husika.”

Kufikia sasa, tayari msimu huu wa Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) umefutiliwa mbali huku kukikosekana mshindi, timu zilizoteremshwa ngazi wala kupandishwa daraja.

Japo Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) imepangwa kurejelewa wakati wowote kuanzia Mei 16, dalili zote zinaashiria uwezekano wa kufutiliwa mbali kwa msimu huu mzima katika kampeni za kuwania ufalme wa kipute hicho.

Vinara wa Uefa wamesisitiza kwamba huenda wakalazimika kutumia matokeo ya hadi kufikia sasa kuamua vikosi vitakavyoshiriki kipute cha Klabu Bingwa muhula ujao.

Iwapo misimu kadhaa ya ligi haitakamilika kutokana na virusi vya corona, itajuzu mashirikisho husika ya mataifa mbalimbali kubuni mbinu zitakazowaongoza kuteua vikosi vitakavyonogesha kampeni za UEFA msimu ujao.