Michezo

Ligi ya Japan yakosa kisa cha corona

September 18th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LIGI ya Soka Japan (J League) haijapata kisa chochote cha maambukizi ya virusi vya corona katika zoezi lake la hivi punde la kupima washiriki baada ya kupima watu 3,245 wakiwemo wachezaji na marefa.

Mkenya Michael Olunga anachezea Kashiwa Reysol katika J1 League inayojumuisha timu 18.

Shughuli ya kupima wachezaji na maafisa wanaoshiriki ligi hiyo ilianza Juni 18, wiki mbili baada ya michezo kurudi viwanjani, huku maelfu wakipimwa na wanaopatikana na virusi hivyo kutengwa na kupokea matibabu.

Raundi ya Julai 29 hadi Agosti 2 ilishuhudia visa vitatu vya maambukizi ya virusi hivyo kutokana na watu 3,203 waliopimwa. Kisa kimoja pia kiliripotiwa katika raundi ya tano ya upimaji wa watu 177 kati ya Agosti 13 na Agosti 24, huku klabu ya Sagan Tosu ikiathirika baada ya meneja wa timu hiyo Kim Myung-hwi kupatikana na virusi hivyo. Timu hiyo wakati mmoja ilisemekana kuwa na visa tisa vya maambukizi ya virusi hivyo na kusimamisha shughuli zake zote kwa muda.

Tosu ilirejea uwanjani Septemba 5 na tangu wakati huo imezoa ushindi mara mbili ikiwemo kupiga Kashiwa 2-1 (Septemba 13), kutoka sare mara moja na kupoteza mchuano mmoja.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE