Michezo

Ligi ya Olunga yaahirishwa kwa sababu ya coronavirus

February 25th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

JAPAN imetangaza Februari 25 kusimamisha mechi zote za Ligi Kuu (J-League) na mashindano mengine kwa sababu ya tishio la ugonjwa hatari wa Coronavirus.

Mshambuliaji matata wa Kenya, Michael Olunga ameajiriwa na Kashiwa Reysol iliyoingia Ligi Kuu msimu huu.

Tayari mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameifungia mabao matatu. Alipata bao moja Kashiwa ikianza msimu kwa kupepeta Gamba Osaka 1-0 katika Levain Cup (League Cup) mnamo Februari 16 na kupachika mawili ikilemea Consadole Sapporo 4-2 ligini mnamo Februari 22.

Taarifa kutoka nchini Japan zinasema kuwa hali ya kawaida itarejelewa Machi katikati, huku Japan ikiungana na Uchina na Korea Kusini katika kusimamisha mashindano ya soka ili kukabiliana na mkurupuko huo, ambao umeathiri watu 80,000 kote duniani na kuua 2,700.

“J-League imeamua kufanya uamuzi mkubwa kuhusu kusambaa kwa maambukizi ya visa vipya vya Coronavirus,” mwenyekiti wa ligi hiyo Mitsuru Murai ameeleza wanahabari Jumanne.

“Tumeamua kuahirisha mechi za Levain Cup zilizoratibiwa kusakatwa Februari 26 pamoja na mashindano yote rasmi hadi Machi 15.”

Ikisalia miezi mitano michezo ya Olimpiki ianze mjini Tokyo nchini Japan, virusi hivyo pia vimezua hofu. Maandalizi ya mashindano hayo yameathiriwa kwa njia tofauti ikiwemo kusimamisha shughuli ya kufunza waelekezi wa kujitolea.

Vilevile, mbio za Tokyo Marathon zilizoratibiwa kufanyika Machi 1 zitaendelea jinsi zilivyopangwa, lakini zikihusisha tu wakimbiaji watajika.