Michezo

Ligi yatamatika kwa mbio za mfungaji bora

May 29th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPENGA cha kuashiria tamati ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu huu kitapulizwa leo Jumatano huku jumla ya mechi tisa zikipangiwa kuanza kwa wakati mmoja; saa nane mchana (2p.m.) katika viwanja mbalimbali nchini.

Gor Mahia tayari wametawazwa mabingwa wa muhula huu baada ya kutia kapuni ubingwa wa KPL kwa mara ya 18 katika historia ya kivumbi hicho.

Vihiga United na Mount Kenya United wameteremshwa ngazi kutoka KPL na hivyo, watashiriki kipute cha Ligi ya Taifa ya Supa (NSL) msimu ujao.

Vita vya kuwania taji la mfungaji bora ndivyo vitakavyochacha huku Chemelil Sugar, Posta Rangers na Zoo Kericho zikipigania fursa ya kusalia ligini msimu ujao.

Kufikia sasa, nyota Allan Wanga wa Kakamega Homeboyz anaongoza orodha ya wafungaji bora kwa jumla ya mabao 18, moja zaidi kuliko Umaru Kasumba wa Sofapaka na Enosh Ochieng anayevalia jezi za mabingwa mara nne, Ulinzi Stars.

Kikosi kitakachokamata nafasi ya 16 katika jedwali la Ligi Kuu ya KPL kitajikatia tiketi ya kushiriki mchujo dhidi ya kikosi kitakachomaliza kampeni za NSL katika nafasi ya tatu.

Mshindi wa mchujo huo wa mikondo miwili atafuzu kwa KPL muhula ujao huku kikosi kitakachozidiwa maarifa kikisalia kushiriki NSL.

Rangers na Zoo wako bega kwa bega kwa alama 32 katika nafasi za 14 na 15 mtawalia, alama moja mbele ya Chemelil wanaokamata nafasi ya 16.

Tusker FC yaikaribisha Rangers

Rangers watakuwa wageni wa Tusker FC hii ugani Ruaraka huku Zoo na Chemelil wakitazamiwa kushinda mechi zao dhidi ya KCB na SoNy Sugar mtawalia. Chemelil watawaalika mabingwa wa 2006, SoNy ugani Chemelil Sports Complex nao KCB wavaane na Zoo mjini Mumias.

Ilivyo, ni Chemelil ndio walioko katika hatari zaidi ya kukutana na mmoja kutoka orodha ya Kisumu All Stars, Nairobi Stima, Ushuru, Kenya Police, Bidco United na Talanta zinazoweza kumaliza Ligi ya NSL katika nafasi ya tatu muhula huu.

Chemelil, ambayo haina ushindi katika mechi nane zilizopita msimu huu, haijashinda SoNy katika jumla ya michuano minne iliyopita.