Michezo

Ligi yatarajiwa kuanza ila kombe la kuwaniwa halijanunuliwa

August 8th, 2019 2 min read

Na CECIL ODONGO

HUKU yakisalia majuma mawili pekee kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kuanza, kampuni inayoendesha ligi hiyo bado haijanunua kombe jipya la kuwaniwa na klabu 18 zinazoshiriki kipute hicho.

Mwenyekiti wa KPL Jack Oguda alieleza kuwa wadhamini wa ligi hiyo, SportPesa bado wanaendelea kuirai serikali kubatilisha agizo la kuzimwa kwa biashara zake nchini na ni baada ya hapo ambapo kombe hilo litanunuliwa.

“Kwa sasa bado tunasubiri japo siku zinazidi kusonga na kulingana na sheria, kombe hilo lazima linunuliwe kabla ya msimu wa 2019/20 kung’oa nanga Agosti 30. Linagharimu Sh1 milioni na tuna matumaini ya kulipata baada ya utata kati ya SportPesa na serikali kutatuliwa,” Oguda akasema kwenye mahojiano.

Aidha, alibainisha kwamba hawawezi kukumbatia mdhamini mpya kwa sababu SportPesa bado inamiliki, kisheria, haki ya kutumia jina la KPL na tayari imelipa ada ya kupeperushwa kwa mechi kadhaa za ligi hiyo.

“Tumekuwa tukishauriana na kampuni nyinginezo kuona iwapo zitachukua jukumu la kufadhili ligi lakini hatujaafikiana. SportPesa wameonyesha nia ya kuendelea kudhamani KPL na hata wamelipia fedha za kugharimia upeperushaji wa mechi. Tunasubiri washauriane na serikali kisha wamalize sehemu iliyosalia ya ufadhili na kununua kombe,” akaongeza Oguda.

KPL imelazimika kununua kombe jingine baada ya mabingwa mara 18 Gor Mahia kushinda taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo kuanzia mwaka wa 2017, 2018 na 2019.

Hii itakuwa mara ya pili kampuni hiyo kuhitajika kununua kombe jipya tangu 2010, ya juzi kabisa ikiwa mwaka wa 2016 ilipolazimika kujitosa sokoni baada ya Gor kulishinda kuanzia 2013 hadi 2015.

Afisa huyo vilevile alikiri kwamba itakuwa vigumu kwa KPL kuongeza Sh4.5 milioni ambazo mshindi wa ligi hutunukiwa, akisema pandushuka za kifedha na masaibu yanayowakumba wafadhili hao yanadidimizi kupandishwa kwa kiwango cha sasa.

“Bajeti yetu sasa imebanwa kabisa ukizingatia hali ya sasa ya kiuchumi na masaibu yanayowakumba wafadhili wetu. Tulikuwa tumetafakari kuhusu nyongeza hiyo hasa baada ya malalamishi kutanda kwamba kiasi hicho ni cha chini mno lakini tuna matumaini hali itabadilika na ipo siku hayo yatatimia,” akasema Oguda.

Msimu mpya wa KPL utaanza Jumamosi Agosti 30 kwa mechi kati ya Kariobangi Sharks na Western Stima.

Mechi tano zitasakatwa siku inayofuatia na nyingine tatu siku ya Jumatatu Septemba 1, 2019.