Makala

LILA NYOKABI: Serikali isaidie kuinua vipaji kutoka familia maskini

November 14th, 2020 2 min read

NA JOHN KIMWERE

Ni kati ya wasanii chipukizi wanaojiwekea matamanio ya kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo. Lila Esther Nyokabi ni kati ya wasanii wanaokuja ambao tayari wamepania kujituma kiume katika masuala ya maigizo hapa nchini.

Msichana huyu ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN). Binti huyu aliyezaliwa mwaka 1999 anasema ingawa ndio mwanzo wa ngoma ana imani atafanya kweli katika tasnia ya uigizaji miaka ijayo.

”Binafsi nahisi nina kipaji cha uigizaji jambo lililochangia kuanza kujituma katika masuala hayo mwaka 2017,” alisema na kuongeza kuwa anafahamu changamoto anazotarajia kukubana nazo katika sekta hiyo.

Ingawa alidhamiria kuwa mwigizaji tangia akiwa mtoto anasema alipata motisha ya kushiriki uigizaji alipotazama msanii Nyce Wanjeri aliyepata umaarufu kupitia filamu ya Auntie Boss iliyokuwa ikipeperushwa kupitia runinga ya NTV.

Nyokabi aliyezaliwa katika Kaunti ya Nyeri anasema alianza kushiriki uigizaji chini ya kundi la Kenya Viners chuoni humo. Chini ya kundi hilo anajivunia kushiriki komedi kadhaa ambazo huonyeshwa kupitia mtandao ya Youtube. Baadhi yazo ni kama: ‘Chicken soup for the 20year old soul,’ ‘When you bring your A game but your tongue,’ na ‘When the invigilat or leaves the room.’

”Katika mpango mzima ninalenga kushiriki filamu nzuri zitaopata mpenyo kuonyesha kwenye runinga,” anasema na kuongeza kila wakati msanii yeyote huwa na matamanio ya kufanya vizuri.

Msichana huyo anasema anaamini uigizaji ni ajira kama zingine ambapo amepania kukaza buti huku akilenga kutinga upeo wa mwigizaji wa kimataifa mzawa wa Kenya, Lupita Nyong’o. Dada huyu anayetamba katika filamu za Hollywood anajivunia kushiriki filamu zilizopata umaarufu sio haba ikiwamo Black Panther na 12 Years a Slave.

”Serikali inastahili kusaidia vijana kutoka familia maskini hasa wenye talanta mbali mbali ili kujijengea maisha ya siku sijazo,” alisema na kuongeza kuwa taifa hili limefurika vijana wengi wavulana kwa wasichana waliotunikiwa vipaji tofauti kama michezo na uigizaji kati ya zingine.

Katika sekta ya uigizaji hapa nchini dada huyu anasema angependa kufanya kazi na msanii Celestine Gachuhi ambaye hushiriki filamu ya Selina akifahamika kama Selina. Pia Eve D’Souza ambaye hujulikana kama Varshita kwenye filamu ya Auntie Boss.

Ingawa hajapata mashiko katika tasnia ya uigizaji dada huyu sio mchoyo wa mawaidha. Anashauri wasanii wanaokuja kuwa wasife moyo pia wasifikiri uigizaji ni rahisi unahitaji bidii na mwelekeo.