Siasa

Limuru III yazaa muungano wa Haki

May 17th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

WAANDALIZI wa Kongamano la Limuru III ambao ni wanasiasa kutoka Mlima Kenya wanaoegemea mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya Alliance, wametangaza kuzinduliwa kwa muungano wa kisiasa ambao utaunganisha vyama zaidi ya 30.

Wakihutubu mnamo Ijumaa katika ukumbi wa Jumuia mjini Kiambu, wamesema kwamba kuanzia sasa, vyama hivyo vitakuwa vikiwajibikia Muungano wa Haki na ambao mfadhili wake atakuwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Katibu Mkuu wa Jubilee Bw Jeremiah Kioni alitangaza kwamba Bw Kenyatta ndiye atakuwa anawaelekeza na atakuwa akiwaita kwa mkutano ikihitajika licha ya kwamba hakuna wadhifa na majukumu ya kisiasa atakayotekeleza.

“Mnamjua… Yeye ndiye kiongozi wetu na kila akiitisha mkutano kutupa mwelekeo tutakuwa tunatii. Tutategemea busara yake katika mikakati ya kutupeleka mbele,” akasema Bw Kioni.

Bw Kioni aliongoza wajumbe kuidhinisha maazimio ya Limuru III ambayo ni kuungana na kuongea kwa sauti moja, kuhakikisha wapigakura 9 milioni 9 watampigia mmoja wao kutoka jamii za Gikuyu, Embu na Meru katika uchaguzi wa 2027 na pia kushinikiza utawala wa Rais William Ruto ukome kutoza ushuru kiholela.

Kiongozi wa Narc Kenya Bi Martha Karua ambaye alikuwa mshirikishi mwenza wa kongamano hilo, aliwataka wenyeji kukaa pamoja na kwa upendo huku wakijaliana masilahi.

Bi Karua alidai kwamba kwa sasa utawala wa Rais Ruto umegeuka kuwa kidonda kwa wenyeji wa Mlima Kenya ambao kila uchao, wanapoteza uwekezaji kutokana na ushuru wa juu.

Alimtaka Dkt Ruto awahamishie waathiriwa wa mafuriko katika nyumba zilizokamilika chini ya mradi wa makao ya bei nafuu kwa kuwa zimejengwa katika ardhi ya umma kwa kutumia ushuru wa lazima kutoka kwa Wakenya.

Azimio jingine lililopitishwa ni la kutetea ugavi wa rasilimali na mamlaka ya kisiasa kupitia kigezo cha idadi ya watu.

Bi Karua alisema kwamba kuna maeneobunge na kaunti–nje ya Mlima Kenya–ambako kuna idadi ndogo ya wakazi lakini hupewa migao ya juu kuliko Mlima Kenya yenye idadi kubwa ya watu.

“Wakati wanataka kutukandamiza, huwa wanatuita wakabila tunapokutana. Sasa waelewe kwamba tutaanza vikao katika kila kaunti ili tuongee kuhusu yanayotuhusu tukijiandaa kung’oa utawala huu wa sasa kutoka mamlakani mwaka 2027,” akasema Bi Karua.

Aidha, waliohutubu walisema wamekataa katakata misako dhidi ya vijana wa eneo hilo kwa msingi wa kupambana na kundi haramu la Mungiki.

Kongamano hilo ambalo lilitatarajiwa kuwaleta pamoja vigogo wa siasa za upinzani Mlima Kenya halikuafikia matarajio hayo, wengi wakilisusia.

Wandani sugu wa Bw Kenyatta kama aliyekuwa Gavana wa Meru Bw Peter Munya, aliyekuwa Waziri wa Afya Bw Mutahi Kagwe, aliyekuwa Gavana wa Murang’a Bw Mwangi wa Iria na aliyekuwa Waziri wa Maji Sicily Kariuki, walikuwa miongoni mwa waliokuwa wakitarajiwa kufika lakini wakakosa.

Aidha, wanamuziki wa eneo la Mlima Kenya walisusia licha ya kuwa kiungo thabiti cha Bw Kenyatta katika siasa za 2022.

Kinaya ni kwamba, washirikishi wa kongamano hilo kupitia hotuba zao walisema wanajuta kuachilia uwaniaji wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Walisema walihadaiwa hadi Dkt Ruto akapenya Mlima Kenya na kuchota kura za ushindi zilizopokonya eneo hilo ukiritimba wa kutawala Kenya.

Lakini hata Dkt Ruto angekosa kuibuka mshindi wa urais, aliyekuwa apate ni Bw Raila Odinga ambaye pia sio mzawa wa Mlima Kenya.

Wadadisi sasa wakisema kongamano hilo la Limuru III ni njama mpya ya kumponda Dkt Ruto na kufufua harakati za kumpa Bw Kenyatta ushawishi hata akiwa ameshastaafu.