Michezo

Lindelof asema hana haja na kuhamia Nou Camp

July 16th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

BEKI wa Manchester United Victor Lindelof amepuuza uvumi unaomhusisha na uhamisho hadi kambini mwa vigogo wa soka nchini Uhispania, Barcelona, akisema kwa sasa anayafurahia maisha ugani Old Trafford.

Agenti wa mwanadimba huyo Hasan Cetinkaya ndiye aliibua madai hayi ya uhamisho wiki jana kwa kusema kwamba kusalia kwa mteja wake Old Trafford, kunategemea jinsi atakavyoafikiana na waajiri wake.

Madai hayo yalijiri baada ya tetesi kuzagaa kwamba Barcelona walikuwa na nia ya kumsajili Lindelof iwapo wangekosa saini ya beki raia wa Uholanzi Mathjis De Light.

Lindelof, raia wa Uswidi alipuuza uvumi kuhusu uhamisho wake wakati Manchester United inaendelea na mazoezi makali kabla kivumbi cha kufa mtu dhidi ya Leeds FC jijini Perth nchi Australia Jumatano Julai 17. Mwanadimba huyo chipukizi alisema tayari anawaza jinsi atakavyovumisha timu yake msimu wa 2019/20 unaoanza mwezi Agosti.

“Huwa ninafurahi kuitwa mchezaji wa Manchester United kwa kuwa msimu jana wa 2018/19 ulikuwa wenye ufanisi sana kwangu. Nilitamba kuliko ule uliotangulia wa 2017/18 ambao ulikuwa wangu wa kwanza ugani Old Trafford. Huwa ninajibidisha kila siku nikiwa na nia ya kuifanya klabu yangu ing’ae kwenye mashindano mbalimbali,” akasema Lindelof katika kikao na wanahabari.

Lindelof ambaye bado hajaonja uhasama wa tangu jadi kati ya Man United na Leeds FC inayonolewa na kocha Marcelo Bielsa alisema anasubiri mtanange huo ambao utasakatwa kwenye uwanja wa kihistoria Optus kwa hamu na hamumu. Uwanja wa Optus una uwezo wa kuwasitiri mashabiki 60,000 na unatarajiwa kujaa hadi pomoni wakati wa mechi kati ya timu hizo mbili.

“Kwa kweli nafahamu uhasama na historia wa miaka nenda miaka rudi kati ya timu hizi. Nafikiri mechi hiyo itakuwa ngumu na naisubiri kwa hamu kuu,” akaongeza mwanadimba huyo aliyejiunga na Man United mwaka wa 2017 kutoka Benfica ya Ureno.