Michezo

Lingard ni kichekesho kingine pale Old Trafford

May 20th, 2019 2 min read

NA JOB MOKAYA

BEKI wa kulia wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold amekuwa mchezaji aliyeisaidia sana Liverpool msimu huu hadi kuichochea timu yake kumaliza ya pili kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Manchester City chini ya Pep Guardiola ilimaliza ya kwanza. Trent mwenye umri wa miaka 20 na raia wa Uingereza, alitoa pasi 12 zilizozalisha magoli katika mechi za EPL msimu huu pekee. Liverpool ilifunga msimu kwa pointi 97, alama moja nyuma ya mabingwa Man-City waliojizolea alama 98.

Ni Eden Hazard, mshambulizi wa Chelsea, na Ryan Fraser anayewasakatia AFC Bournemouth ndio wa wapekee waliochangia mabao mengi zaidi kuliko Trent.

Ikumbukwe kwamba Trent ni difenda ilihali wawili hawa ni mastraika. Hapa, Trent anaishia kumwaibisha sana Jesse Lingard, mshambulizi wa Man-United ambaye ametoa krosi mbili pekee zilizosababisha mabao msimu huu.

La kushangaza zaidi ni kwamba Alexander-Anord amechangia magoli mengi kwa mechi 29 alizocheza msimu huu zaidi ya Lingard alivyofanya katika miaka yote aliyocheza soka.

Je, unakumbuka ile krosi aliyoitoa Anfield wakati wa mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Barcelona? Trent aliupokea mpira na kuelekea kupiga kona zikiwa zimesalia dakika za kuku kumeza punje mtanange kutia nanga.

Mchezaji huyu wa Liverpool aliutega mpira kwenye kitovu cha kupigia kona. Kisha akawa anatembea kana kwamba anamwachia mchezaji mwenzake apige kona hiyo.

Wachezaji wa Barcelona wakawa wamezubaa. Kisha akarudi mbio wakati mabeki wa Barcelona wameshika viuno na kutoa krosi ya chini kwa chini iliyompata Mkenya anayechezea Ubelgiji Divock Origi aliyefunga bao la nne. Siku hiyo pekee, Trent alitoa krosi mbili zilizosababisha magoli.

Kwa upande wake, Lingard amechangia magoli 10 wakati wake wote wa taluuma, katika mechi 111 alizocheza. Takwimu hizi zinamfanya Lingard aonekane kichekesho kikubwa akilinganishwa na difenda aliyecheza mechi 29 pekee.

Aidha, Lingard amecheza kwa miaka sita katika kiwango cha juu huku Trent akiwa amecheza miaka miwili pekee. Aibu iliyoje! Msimu huu, Lingard amechangia krosi mbili pekee zilizosababisha magoli mawili hii ikiwa ni aibu kubwa kwa mchezaji ambaye ni mshambuliaji.

Aidha, Lingard, mwenye umri wa miaka 26, amefunga mabao manne pekee msimu huu na kuisaidia Man-United kumaliza kampeni za EPL katika nafasi ya sita.

Ulinganuzi huu unadhihirisha namna Man-United ilivyokuwa duni msimu huu ingawa pia unadhihirishwa namna chipukizi huyu wa Liverpool alivyokuwa mzuri katika nafasi yake.

Lingard alitajwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza itakayoshiriki michuano ya mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League). Mashabiki wengi walishangaa ni kwa nini mchezaji ambaye hakuonyesha lolote la muhimu alitajwa katika kikosi cha Uingereza.

Nyota ya Lingard ilianza kung’aa wakati Jose Mourinho alitua uwanjani Old Trafford. Mourinho alimpenda Lingard kwa utendakazi wake wala si mchezo wake.

Utendakazi wa Lingard ni sawa na wa punda. Hachoki. Ndio maana Mourinho alimtuma uwanjani kusaidia kikosi kujihami.

na vilevile kusaidia katika kushambulia kwa kushtukiza na kukimbia kwa kasi kisha kufunga bao. Ingawa kocha wa sasa wa Man-United amezidi kumtumia Lingard, matumizi yake hayajazaa matunda mema.