Habari za Kitaifa

Linturi aondolewa mashtaka yote kuhusiana na uuzaji mchanga uliopakiwa kama mbolea

May 13th, 2024 2 min read

NA DAVID MWERE

WAZIRI wa Kilimo Mithika Linturi ameondolewa mashtaka yote kuhusiana na uuzaji wa mchanga ukisemekana kuwa mbolea, huku wabunge wa Upinzani wakilaumu wenzao wa upande wa Serikali katika kamati iliyoteuliwa na bunge.

Wabunge saba kati ya 11 kwenye kamati hiyo, walipiga kura ya kumwokoa Bw Linturi, wakisema kwamba mbunge huyo wa zamani wa Igembe Kusini hakuhusika moja kwa moja katika kashfa hiyo.

Kamati hiyo iliyosimamiwa na Mwakilishi wa Kike wa Marsabit, Bi Naomi Waqo, ilipuuzilia mbali mashtaka yaliyowasilishwa na mbunge wa Bumula, Bw Jack Wanami Wamboka kuhusu sakata ya usambazaji wa mbolea feki.

Hoja yake ilipitishwa na wabunge 149 kati ya 188 waliokuwa bungeni wiki mbili zilizopita. Wabunge 36 waliipinga lakini kamati ikaundwa kufuatilia na kuchunguza madai hayo.

Kwenye hoja yake, Bw Wamboka alitaka Waziri Linturi afutwe kazi kwa kukiuka sheria na katiba. Aliamini kuwa kwa kufanya hivyo, Bw Linturi alitekeleza uhalifu mkubwa chini ya sheria na maadili ya mwenye kushikilia ofisi ya waziri.

Lakini jana mmoja wa wabunge waliokuwa kwenye kamati hiyo, aliambia Taifa Leo kwamba wanachama waliteuliwa kwenye kamati maalumu ya kumchunguza Bw Linturi ‘kwa makini sana’ ili kuhakikisha kuwa wanamuokoa.

“Sina nia ya kuwaharibia majina wabunge wenzangu lakini ukiangalia walioteuliwa kuwakilisha bunge kwenye kamati, utaona wazi wabunge wa upande wa muungano tawala, hawakuteuliwa wachunguze bali walipata maagizo wafanye wawezalo kumuondolea mashtaka,” akasema, bila kutaka ajulikane kwa sasa.

Kamati hiyo kikatiba inahitajika kuwasilisha ripoti yake ndani ya siku 10 tangu kuundwa. Ilikamilisha vikao vyake Ijumaa na kwenda katika hoteli ya Argyle barabara ya Mombasa, kuandika ripoti kabla ya kikao maalumu cha bunge leo.

Kifungu cha 152 (9) cha katiba kinasema; “Iwapo ripoti ya kamati maalumu itaonyesha madai hayajathibitishwa, hakutakuwa na haja ya kuchukua hatua zaidi,” ikiwa na maana kuwa suala hilo limekufa na kamwe haliwezi kurejeshwa wakati wa kipindi cha sasa cha bunge.

Kama madai hayo yangeidhinishwa, Bunge lingempa waziri huyo fursa ya kujieleza na kisha kura ipigwe wabunge wote wakiwepo. Ni wabunge 176 wanaohitajika kupitisha suala hilo ili waziri awe amefutwa kazi.

Jana, kiongozi wa Wachache, Bw Opiyo Wandayi alisema kwa kuwa hajaiona ripoti hiyo, hawezi kuizungumzia.

“Bunge liliwapa wanakamati mamlaka huru. Baadhi yetu tunaisubiri ripoti iletwe rasmi bungeni kabla ya kuzungumza zaidi,” akasema mbunge huyo wa Ugunja.

“Bunge lilitoa kauli yake wazi pale wabunge 149 walipopitisha kauli ya kutokuwa na imani na Waziri Linturi. Chochote kitakachofuata baada ya hapo, ni maelezo tu,” akaongeza.

Wabunge walio kwenye kamati iliyomchunguza Waziri Linturi, ni Bi Waqo, Naibu Kiranja wa Wengi Samuel Chepkong’a (UDA, Ainabkoi), George Murugara (UDA, Tharaka), Malulu Injendi (ANC, Malava), Mwakilishi wa Kike wa Kirinyaga Njeri Maina (UDA), na mbunge wa Matuga Kassim Tandaza (ANC).

Upande wa Azimio uliwakilishwa na Naibu Kinara wa Wachache Robert Mbui (Wiper, Kathiani), Tom Kajwang’ (ODM, Ruaraka), Catherine Omanyo (ODM, Mwakilishi wa Kike, Busia) na Yusuf Farah (ODM, Wajir Magharibi).