Habari za Kitaifa

Linturi sasa akodolea shoka na macho baada ya hoja ya kumtimua kukubalika Bungeni

April 30th, 2024 1 min read

Na CHARLES WASONGA

HATIMA ya Waziri wa Kilimo Mithika Linturi katika baraza la mawaziri wa serikali ya Rais William Ruto sasa itaamuliwa na wabunge Alhamisi watakapojadili na kuipigia kura hoja ya kutimuliwa kwake.

Hii ni baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula Jumanne kuidhinisha hoja hiyo inayodhaminiwa na Mbunge wa Bumula Jack Wamboka Wanami akimsuta Linturi kuhusiana na uagizaji na uuzaji wa mbolea feki.

“Hoja hii imetimiza mahitaji ya kikatiba na sheria za bunge na hivyo imeidhinishwa kujadiliwa rasmi na hatima yake kuamuliwa,” Spika Wetang’ula akasema bungeni jana kwenye taarifa yake kuhusu hoja hiyo.

Bw Wanami, aliwasilisha hoja hiyo kwa afisi ya Spika mnamo Jumatano wiki jana akiiandamanisha na sahihi za wabunge 110 wanaoiunga mkono.

Wabunge hao wanatoka mirengo ya muungano tawala wa Kenya Kwanza na ule wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya.

Miongoni mwa wabunge hao ni Joyce Kamene (Machakos, Wiper), Raphael Wanjala (Budalangi, ODM), Pauline Lenguris (Samburu MP, UDA), Maryanne Kitany (Aldai, UDA), Adams Korir (Keiyo North, UDA), Otiende Amollo (Rarieda, ODM), Samuel Parashina (Kajiado South, ODM), Adagala Beatrice (Vihiga MP, ANC), Stephen Mogaka (Mugirango Magharibi, Jubilee ) na Clive Gisairo (Kitutu Masaba, ODM).