Lionel Messi afunga mabao mawili na kusaidia Argentina kuzamisha Jamaica

Lionel Messi afunga mabao mawili na kusaidia Argentina kuzamisha Jamaica

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alishinda mchuano wake wa 100 kimataifa kwa kufunga mabao mawili yaliyosaidia Argentina kupepeta Jamaica 3-0 mnamo Jumanne usiku.

Ushindi huo uliendeleza rekodi ya kutoshindwa kwa Argentina katika jumla ya mechi 35 mfululizo. Mabingwa hao mara mbili wa Kombe la Dunia wamesalia sasa na mechi mbili pekee ili kufikia rekodi ya dunia inayoshikiliwa na Italia ya kutoshindwa katika michuano 37 mfululizo.

Fowadi wa Manchester City, Julian Alvarez aliwaweka Argentina kifua mbele dhidi ya Jamaica baada ya kushirikiana vilivyo na Lautaro Martinez.

Messi, 35, aliyeingia ugani katika dakika ya 56, alifunga mabao mawili ya haraka yaliyozamisha kabisa chombo cha wageni wao.

Nyota huyo wa Paris St-Germain (PSG) aliyefunga mabao mawili dhidi ya Hunduras katika mchuano wa awali, sasa anajivunia jumla ya magoli 90 kutokana na mechi 164 ndani ya jezi za Argentina.

Pambano dhidi ya Jamaica lilikuwa la mwisho kwa Argentina kutandaza kabla ya kuelekea Qatar kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika kati ya Novemba na Disemba 2022.

Miamba hao wanaopigiwa upatu wa kutwaa Kombe la Dunia, watafungua kampeni zao nchini Qatar dhidi ya Saudi Arabia mnamo Novemba 22, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Maonyesho ya kilimo na biashara yanoga jijini Nairobi

NDIVYO SIVYO: Ni kosa kusema ‘gwara’, unafaa kusema...

T L