Lionel Messi akubali kusalia Barcelona kwa mshahara uliopunguzwa kwa asilimia 50

Lionel Messi akubali kusalia Barcelona kwa mshahara uliopunguzwa kwa asilimia 50

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi amekubali kusalia Barcelona kwa mkataba mpya wa miaka mitano ila kwa mshahara ambao ni nusu ya ujira aliokuwa akipokezwa na miamba hao wa soka ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Ili kumudu mshahara mpya wa Messi, Barcelona pia wamefichua mpango wa kuagana na idadi kubwa ya wanasoka wao kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa msimu mpya wa 2021-22 kupulizwa.

Messi, 34, alisalia mchezaji huru baada ya kandarasi yake na Barcelona kutamatika rasmi mnamo Juni 30, 2021.

Kwa mujibu wa mkataba huo wa zamani, fowadi na nahodha huyo wa timu ya taifa ya Argentina alikuwa akipokezwa ujira wa hadi Sh1.9 bilioni mwishoni mwa kila msimu.

Messi kwa sasa angali likizoni baada ya kuongoza Argentina kutia kapuni ubingwa wa Copa America mnamo Julai 10, 2021 nchini Brazil. Anatarajiwa kutia saini mkataba mpya na Barcelona wakati wowote kuanzia sasa.

Kulingana na mkataba huo mpya, Messi atakuwa huru kubanduka Barcelona na kutafuta hifadhi kwingineko baada ya miaka miwili.

Baadhi ya mikakati ambayo imefichuliwa na rais Joan Laporta katika juhudi za kupunguza gharama ya matumizi ya fedha kambini mwa Barcelona ni kuwatia mnadani wanasoka Antoine Griezmann na kiungo Saul Niguez.

Kikosi hicho tayari kimeagana na wachezaji Junior Firpo, Jean-Clair Todibo na Carles Alena ili kufanikisha mpango huo.

Kabla ya kuhiari kusalia Barcelona, Messi alikuwa akihusishwa pakubwa na Paris Saint-Germain (PSG), Manchester City na vikosi kadhaa vya Major League Soccer (MLS).

Messi ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Barcelona, anajivunia mabao 672 na amenyanyulia kikosi hicho mataji 10 ya La Liga, manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na saba ya Copa del Rey. Aidha, ametawazwa mshindi wa taji la Ballon d’Or mara sita.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

NDONDI: Ajowi kupanda ulingoni Julai 24 kwenye Olimpiki 2020

TAHARIRI: Sekta ya uchukuzi ikombolewe sasa