Michezo

Lionesses kujaribu bahati tena ya kufuzu kushiriki Raga ya Dunia

March 13th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

DROO ya mechi za kufuzu kushiriki Raga ya Dunia ya wachezaji saba kila upande ya Wanawake mwaka 2019 imetangazwa, huku Lionesses ya Kenya ikitiwa katika kundi moja na majirani Uganda pamoja na Papua New Guinea na wenyeji Hong Kong.

Mchujo huu unatarajiwa kuandaliwa mwezi ujao mjini Hong Kong ambapo mshindi atajikatia tiketi ya kujumuishwa katika duru zote za msimu 2019-2020.

Lionesses ilicharaza Uganda 29-7 Mei mwaka 2018 katika fainali ya Kombe la Afrika mjini Gaborone, Botswana. Hata hivyo, majirani hawa wawili, ambao pia ni mahasimu wakubwa, wote walifuzu kushiriki mchujo wa Hong Kong kwa kumaliza kombe hilo katika nafasi hizo mbili za kwanza.

Kenya itakuwa ikijaribu bahati tena ya kuingia Raga ya Dunia baada ya kulemewa 12-7 na mahasimu wao wengine wa tangu jadi Afrika Kusini katika nusu-fainali mjini Hong Kong mnamo Aprili 6 mwaka 2018.

Wakenya watahitaji kujikakamua vilivyo hasa baada ya kufanya vibaya mwezi Desemba katika mashindano ya mwaliko ya Dubai walipovuta mkia baada ya kuchapwa 17-5 na Fiji katika mechi ya kuamua nambari 11 na 12 (mwisho).

Lionesses, Papua New Guinea, Hong Kong na Uganda wako Kundi B. Kundi A linaleta pamoja Japan, Ubelgiji, Scotland na Mexico. Kundi C, ambalo ndilo la mwisho, linajumuisha Brazil, Argentina, Kazakhstan na Poland.