Michezo

Lionesses kukabana na Senegal raga

May 26th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Lionesses itaanza kampeni ya kutafuta ubingwa wa Afrika kwenye mashindano ya Afrika ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanawake dhidi ya Senegal hapo Mei 26, 2018.

Katika ratiba iliyotangazwa na Shirikisho la Raga la Afrika (CAR) Mei 23, 2018, Lionesses ya kocha Kevin Wambua itakamilisha mechi zake za Kundi A dhidi ya Madagascar.

Warembo wa Wambua wanafahamu sana Senegal na Madagascar.

Walirarua Madagascar 27-5 na Senegal 38-0 katika mechi za makundi katika makala yaliyopita nchini Tunisia. Ilibwaga Madagascar 38-0 zilipokutana katika mechi za makundi mwaka 2016.

Katika makala ya mwaka 2015, Lionesses pia ilikanyaga Senegal na Madagascar. Ilinyamazisha Senegal 52-0 na kucharaza Madagascar 33-0. Kenya ilimenyana na timu hizi katika mechi za makundi mwaka 2014, huku ikipepeta Madagascar 24-14 na Senegal 22-0.

Kenya ilizaba Senegal 29-7 katika mechi za makundi mwaka 2013 kombe hili lilipoandaliwa nchini Kenya kwa mara ya kwanza.

Timu hizi pia zilikutana katika makala ya mwaka 2012 ambapo Kenya ililemea Senegal 7-0 katika nusu-fainali. Mwaka 2011, Kenya ililima Madagascar 29-10 katika mechi ya makundi.

Kombe hili litapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya Kwese, ambaye ilisaini kandarasi na Shirikisho la Raga la Afrika (CAR) mwaka 2017.

Mshindi atatawazwa bingwa wa Afrika. Timu zitakazonyakua medali za dhahabu na fedha pia zitaingia mchujo wa kuwania nafasi ya kushiriki Raga ya Dunia mwaka 2018.

Kwingineko, tarehe za mashindano ya kitaifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya, zimetangazwa.

Duru ya Prinsloo Sevens itafungua msimu hapo Julai 21-22 mjini Nakuru. Itafuatiwa na Sepetuka Sevens (Julai 28-29, Eldoret), Kabeberi Sevens (Agosti 18-19, Nairobi), Driftwood Sevens (Agosti 25-26, Mombasa), Dala Sevens (Septemba 8-9, Kisumu) na kufikia kilele katika duru ya Christie Sevens (Sepetamba 15-16, Nairobi).

Ratiba ya Kombe la Afrika la Wanawake:

Mei 26, 2018

Kundi A – Madagascar vs. Senegal (11.08am)

Kundi B – Uganda vs. Zimbabwe (11.30am)

Kundi C – Morocco vs. Zambia (11.52am)

Kundi A – Kenya vs. Senegal (12.44pm)

Kundi B – Tunisia vs. Zimbabwe (1.06pm)

Kundi C – Botswana vs. Mauritius (1.28pm)

Kundi A – Kenya vs. Madagascar (2.20pm)

Kundi B – Tunisia vs. Uganda (2.42pm)

Mei 27, 2018

Robo-fainali (10.30am – 11.36am)

Nusu-fainali (1.26pm – 1.48pm)

Fainali (4.22pm)