Michezo

Lionesses kuleta ubingwa nyumbani

May 28th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wapya wa Bara Afrika wa raga ya wachezaji saba kila upande, Kenya Lionesses, wanatarajiwa nchini Jumatatu jioni kutoka Botswana.

Warembo wa kocha Kevin Wambua walishinda mechi zao zote katika ziara yao ya Gaborone na kutwaa taji hili kwa mara ya kwanza kabisa katika historia yao.

Lionesses, ambayo ilipoteza dhidi ya Tunisia katika fainali ya mwaka 2012 na kulemewa na Afrika Kusini katika fainali ya mwaka 2014, 2015, 2016 na 2017, walipapura Uganda 29-7 katika fainali.

Walianza kampeni yao kwa kunyuka Senegal 41-0 na Madagascar 42-0 katika Kundi A hapo Mei 26.

Wakenya waliendeleza ukatili wao katika ya siku ya pili na mwisho walipozima Zambia 43-7 katika robo-fainali na kucharaza Madagascar 27-0 katika nusu-fainali.

Fainali dhidi ya Uganda ilikuwa ya kusisimua zaidi, huku Kenya ikionyesha makali yake kupitia miguso ya Janet Okelo (miwili), Sinaida Aura (miwili) na mmoja kutoka kwa Linet Moraa.

Grace Adhiambo alipachika mikwaju mitatu. Uganda ilijiliwaza na mguso kutoka kwa Grace Auma na mkwaju wa mguso huo kutoka kwa Charlotte Mudoola.

Afrika Kusini haikushiriki makala haya yaliyoshuhudia Kenya na Uganda zikifuzu kushiriki mchujo wa kuwania tiketi ya kuingia Raga ya Dunia mwaka 2019.