Michezo

Lionesses wasuka njama kuizamisha UG Elgon Cup

June 12th, 2019 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Kenya Lionesses kitakachotegemewa katika kampeni za raga ya wachezaji 15 kila upande mwaka 2019 kimepunguzwa zaidi na kusalia na vipusa 40 baada ya mwezi mmoja wa mazoezi.

Kocha Felix Oloo amekuwa akiwanoa wanaraga 50 kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita katika juhudi za kujisuka vilivyo kwa fainali za Elgon Cup na kampeni za kufuzu kwa Kombe la Dunia mnamo Agosti.

Kama sehemu ya maandalizi baada ya vinara wa Kombe la Dunia kuanzisha mechi za kufuzu kwa kipute hicho, Lionesses walitumia pakubwa kivumbi cha Aberdeen Shikoyi kilichonogeshwa kwa wiki tatu kujipiga msasa.

Oloo alianza safari yake ya kukifua kikosi cha Lionesses akiwa na wachezaji 50 ambao kwa sasa wamepunguzwa hadi 40 baada ya stadi zao mbalimbali katika kila idara kutiwa kwenye mizani chini ya kipindi cha wiki moja iliyopita.

Baada ya wiki tatu zijazo, Oloo anaamini kwamba wanaraga wake watakuwa wameimarika pakubwa kiasi cha kumtatiza mpinzani yeyote atakayekutana nao.

“Kipute cha Elgon Cup kitatupa jukwaa mwafaka la kukadiria kiwango cha maandalizi yetu huku ushindi ukituaminisha zaidi katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Uganda,” akasema Oloo.

Mazoezi

Lionesses hushiriki mazoezi kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa katika uwanja wa RFUEA. Mkondo wa kwanza wa Elgon Cup utapigiwa jijini Kisumu mnamo Juni 22 huku marudiano yakiandaliwa jijini Kampala, Uganda mnamo Julai 13.

Mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitaanza mwezi mmoja baada ya kukamilika kwa kipute cha Elgon Cup na zitapigiwa jijini Johannesburg, Afrika Kusini kati ya Agosti 9-17. Kenya imepangwa katika Kundi A pamoja na Uganda, Madagascar na Afrika Kusini.