Michezo

Lionesses watiwa kundi ngumu Dubai Sevens

October 23rd, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

LIONESSES ya Kenya imetiwa katika ‘kundi la kifo’ kwenye duru ya Dubai Sevens ya Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 itakayoandaliwa Novemba 29-30, 2018.

Mabingwa hawa wa Afrika watamenyana na Ireland, Urusi na New Zealand, ambayo ilishinda duru ya ufunguzi ya Glendale nchini Marekani wikendi ya Oktoba 20-21. Timu hizi ziko katika Kundi A.

Lionesses, ambayo inatarajiwa kupata kocha mpya baada ya Kevin Wambua kuajiriwa katika timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande ya wanaume almaarufu Shujaa, ni timu alikwa. Kundi B linajumuisha wenyeji wa Glendale Sevens Marekani, ambao walikamilisha duru hiyo katika nafasi ya pili, mabingwa wa Dubai Sevens mwaka 2017 Australia pamoja na Uingereza na Uchina.

Canada, Ufaransa, Uhispania na Fiji zimekutanishwa katika Kundi C. Wambua, ambaye Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) lilitangaza mapema mwezi Oktoba kwa ataendelea kuhudumu kama Kocha Mkuu wa Lionesses hadi pale kocha mpya atapatikana, amekiri kundi la Dubai ni ngumu.

Hata hivyo, amesema ni matayarisho mazuri kwa Kenya kabla ya mchujo wa kuingia Raga ya Dunia msimu 2019-2020 pamoja na kuwania tiketi ya kushiriki Olimpiki mwaka 2020 kupitia Kombe la Afrika mwaka 2019.

“Lengo letu kubwa ni kuwa tayari kwa mashindano ya mwaka ujao, ambao ni muhimu sana kwetu kwa sababu tutakuwa na fursa ya kushindania tiketi ya kushiriki Raga ya Dunia pamoja Olimpiki.

“Tunataka kutumia Dubai Sevens kujaribu baadhi ya wachezaji wapya wanaojiunga nasi. Hadi sasa, maandalizi yetu yamekuwa mazuri. Tunataka kuimarisha ujuzi wao kujitayarisha kwa majukumu ya mwaka ujao,” Wambua amesema Jumatatu. Ziara ya Dubai itakuwa ya pili ya Lionesses katika Raga ya Dunia baada ya kushiriki Clermont Sevens nchini Ufaransa mwaka 2016.