Habari MsetoSiasa

Lipeni ushuru bila kulalamika Raila apate mshahara, asema mbunge

September 26th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE Maalum David Ole Sankok amewataka Wakenya kubeba mzigo wa kulipa ushuru mkubwa uliopandishwa bila kulalamika, akiwakumbusha kuwa ni wao wanaopaswa kulipia gharama za kiongozi wa upinzani Raila Odinga, baada ya muafaka walioweka na Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Sankok, ambaye huwakilisha watu wanaoishi na ulemavu katika Bunge la Taifa alisema kuwa tangu muafaka kuwekwa baina ya Raila na Rais Uhuru Kenyatta, gharama za serikali zimeongzeka kwani Raila alikuja na ‘watu wake’ ambao wanalipwa kwa pesa za mlipa ushuru.

Vilevile, aliwakumbusha Wakenya kuwa ni wao waliounga mkono kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa ‘Rais wa wananchi’ na hivyo baadaye akakutana na Rais wa serikali na kuwekelea matakwa yake mezani.

Kwenye video ambayo imekuwa ikizunguka katika mitandao ya kijamii, mbunge huyo aliyeteuliwa kwa tiketi ya chama cha Jubilee sasa anawataka Wakenya kukubali kulipa ushuru wa asilimia nane bila kelele kwa kuwa gharama za serikali kwa sasa ni nyingi mno.

“Nataka kusihi Wakenya kwa heshima kubwa sana, tafadhalini tukubali tulipe ushuru ndio tupate pesa za kulipa Raila Amolo Odinga mshahara, kwa sasbabu nyinyi wenyewe ndio mlienda kumuapisha kuwa ‘Rais wa wananchi’ na huyo Rais wa wananchi akakuja na muafaka (handshake),” Bw Sankok akasema.

Aliongeza kuwa baada ya muafaka imebidi Bw Odinga kuanza kulipwa na serikali na gharama zake za ziara za ndani na nje ya nchi kulipwa na mlipa ushuru.

“Sasa kuna gharama ya juu kuhakikisha ya kwamba anapata mshahara pamoja na watu wake ambao alikuja nao na apate pesa za kutangatanga.

Unajua hata kabla ya muafaka alikuwa anatangatanga mazishi za hapa nchini, lakini baada ya hiyo sasa amehitimu kuwa mwombolezaji wa kimataifa hata anatangatanga mazishi ya huko ng’ambo, na hiyo inahitaji marupurupu mengi,” Bw Sankok akawaelezea Wakenya.

Kwa sababu hii, mbunge huyo aliwataka Wakenya kuwa tayari kuingia mfukoni hata zaidi ili kugharamia matumizi mengi ambayo serikali inayo sasa, ujumbe wake ukikinzana na hadithi za serikali kuwa kupandishwa kwa ushuru kulikuwa kwa sababu ya kufadhili miradi ya maendeleo.

“Kwa hivyo gharama ni kubwa kwa serikali kwa sasa, tujaribu na tukubali kulipa ushuru wa asilimia nane ili hii gharama tuikimu,” akasema.

Vilevile, Bw Sankok aliwakumbusha Wakenya kuwa ni wao waliopitisha katiba ya sasa ambayo ina uwakilishaji wa wananchi kupita kiasi, ambao umepelekea mzigo wa mishahara kupanda kwa viwango vya juu zaidi.

“Wakenya wenyewe pia ndio walipitisha katiba mpya, ambayo imetengeneza waheshimiwa wengi kupita raia, hawa wote wanahitaji kulipwa, wanahitaji ofisi, wanahitaji wafanyakazi na yote ni kutokana na ushuru wa Wakenya.”

Video ya mbunge huyo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, huku Wakenya wakiitazama kwa mshangao na kutoamini, wengine wakichekeshwa na ujumbe wake ambao hawakuutarajia.