Makala

LISHE: Dagaa na karanga

July 30th, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

[email protected]

Muda wa kutayarisha: Dakika 30

Walaji: Watu 3

Vinavyohitajika

 • omena – dagaa – kikombe 1
 • mafuta ya kupikia vijiko 4
 • nyanya 3
 • kitunguu kikubwa
 • pilipili mboga nusu
 • karoti 1
 • dania fungu moja
 • juisi ya limau, kijiko 1
 • biringani 1
 • kitunguu saumu vipande 2 vikubwa
 • nyanya pakiti (Tomato paste) 1
 • karanga za kusaga (peanut butter) vijiko 2
 • pilipili mwendokasi 1 (Habanero chilli)
 • chumvi
 • maji
 • sufuria

 

Vinavyohitajika kuandaa dagaa na karanga. Picha/ Diana Mutheu

 

Jinsi ya kuandaa

Chemsha maji, epua kisha yatumie kuoshea dagaa; waeza kata vichwa vya dagaa ukipenda.

Katika sufuria nyingine weka mafuta yako ya kupikia hadi yapate moto, ongeza kitunguu halafu pika hadi kiwe rangi ya dilishe rangi kisha uongeze kitunguu saumu.

Ongeza dagaa katika sufuria na ukoroge vizuri kisha uache chakula hiki kiive katika mafuta hayo kwa dakika tatu hivi.

Koroga na uongeze chumvi ya kutosha, pilipili yako ya mwendokasi na kijiko kimoja kikubwa cha limau alafu uendelee kukaanga dagaa yako ili kuipa ladha zote.

Ongeza pilipili mboga yako, karoti, biringani (kumbuka kutoa ngozi yake ili iive vizuri), nyanya na ufunike sufuria kwa muda wa dakika nne ili viungo vyako vilainike vizuri. Unaweza kuongeza maji vijiko vinne.

Ongeza kijiko kimoja cha nyanya pakiti, koroga vizuri, kisha uongeze dania yako na ukoroge.

Changanga karanga yako ya kusaga na maji kidogo kisha uiongeze ndani ya sufuria ya dagaa ambazo zimeiva. Acha ichemke kwa sekunde 30 tu- ukiacha zaidi ya hapo, itashikamana sana.

Waeza andaa kwa sima – ugali – na wali.

Furahia.

Dagaa na karanga pamoja na wali. Picha/ Diana Mutheu