Makala

LISHE: Jinsi ya kupika spaghetti na meatballs zilizotiwa jibini

October 17th, 2020 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 10

Muda wa kupika: Dakika 30

Walaji: 2

Vinavyohitajika

 • nusu paketi ya spaghetti
 • kilo ½ ya meatballs
 • nyanya 1
 • kitunguu
 • kijiko 1 cha kitunguu saumu
 • kijiko 1 cha tangawizi
 • kikombe 1 nyanya ya kopo
 • vijiko 2 vya mafuta ya mzeituni
 • kikombe 1 maji
 • ½ kikombe jibini ya mozzarella
 • majani ya giligilani
Meatballs na jibini. Picha/ Margaret Maina

Maelekezo

Weka nyanya na kitunguu kwenye blenda kutengeneza rojo; twanga kitunguu saumu na tangawizi kwa ajili ya kutengeneza sosi, weka kando.

Katakata jibini ya mozzarella vipande vidogovidogo vya umbo la mraba. Katakata pilipili na majani ya giligilani vipande vidogovidogo.

Kwenye sufuria katika moto wa juu kiasi, chemsha mafuta kipimo cha vijiko viwili. Ongeza meatballs. Kaanga kwa muda wa dakika mbili au mpaka ziwe za kahawia kwa nje ila zisiive kabisa.

Meatballs na jibini. Picha/ Margaret Maina

Hamisha nyama kwenye sahani.

Chemsha spaghetti kutokana na maelekezo yaliyoko kwenye paketi; chuja maji halafu weka kando.

Irudishe mekoni sufuria uliotumia kupika nyama. Chemsha hapo mafuta vijiko viwili. Ongeza kitunguu saumu na tangawizi na upike mpaka viive.

Ongeza rojo ya nyanya na nyanya ya kopo; koroga vizuri.

Pika mpaka nyanya ziive vizuri.

Ongeza maji kikombe kimoja; acha yachemke mpaka sosi ianze kutokota.

Ongeza nyama, pika kwa dakika tano au mpaka iive vizuri. Kuwa muangalifu isiive sana.

Ongeza spaghetti zilizochemka; pika kwa dakika zingine mbili.

Weka majani ya giligilani. Epua.

Pakua chakula kiliwe kabla ya kupoa sana.