Makala

LISHE: Jinsi ya kutengeneza aiskrimu 'lambalamba' za maziwa zenye chokoleti juu

October 6th, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

[email protected]

Vinavyohitajika

  • maziwa lita 1
  • maziwa ya unga kikombe 1
  • sukari kiasi vijiko 4
  • corn flour kijiko 1
  • vikombe kadhaa vya aiskrimu
  • vijiti kadhaa vya aiskrimu
  • chokoleti ya kupika iliyokolea rangi (dark) kikombe 1
  • sufuria
  • maji

Jinsi ya kutengeneza

Mimina maziwa yako katika sufuria safi kisha uongeze maziwa ya unga na ukoroga hadi yachemke.

Ongeza sukari na uache mchanganyo huo uendelee kuchemka.

Chukua corn flour yako na uchanganye na maji kiasi kisha uongeze katika maziwa yaliyochemka. Koroga hadi pale mchanganyiko huo utakuwa mzito kabisa. Epua na uache upoe.

Kisha mimina mchanganyiko wako katika vikombe vyako vya aiskrimu na uweke vijiti vyake, kisha uviweke katika sehemu baridi kabisa (freezer) ndani ya jokofu lako.

Chukua chokoleti yako na uzikatekate vipande vidogo vidogo na uviweke katika bakuli nzito ya glasi.

Kisha chemsha maji katika sufuria, epua kisha uweke chokoleti yako juu ya sufuria ili iweze kuyeyuka kwa mvuke wa maji moto. Subiri ipoe kidogo kisha uweke katika kikombe kirefu na kipana.

Aiskrimu yako ikishaganda kabisa, toa kwenye jokofu, kisha moja kwa moja zichovye ndani ya kikombe cha chokoleti ukishika vijiti hivyo haraka haraka kabla zianze kuyeyuka. (chovya kabisa hadi sehemu zote zifunikwe na chokoleti la sivyo, aiskrimu ya ndani itaanza kuyeyuka)

Ukichovya kisha utoe, chokoleti itaganda mara moja.

Furahia na wote unaowaenzi. Kumbuka kula kwa kipimo.