Makala

LISHE NA AFYA: Je, unafahamu manufaa ya mananasi?

March 6th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KWA mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21, nanasi ni tunda lililo na ganda lenye miba na kitita cha majani nchani yenye mibamiba.

Ni mojawapo kati ya matunda yanayopendwa zaidi kutokana na ladha nzuri na tamu ambayo inatokana na sukari iliyoko ndani ya tunda hili.

Mananasi ni matunda ambayo yanatumika sana kutengeneza juisi. Yana pia faida nyingi za kiafya kwenye mwili wa mwanadamu.

Mananasi ni chanzo muhimu sana cha vitamini pamoja na madini ambayo yanasaidia kuimarisha afya ya mwanadamu ambazo ni kama vile Thiamin, Riboflavin, Vitamini B-6 , Folate , Acid ya Pantothenic pamoja na madini ya Magnesium, manganese na potasia.

Mananasi husaidia kutibu vidonda na uvimbe

Kati ya vurutubisho vilivyoko ndani ya nanasi ni Bromelain, ambayo husaidia kuondoa maumivu kwenye viungo, kupunguza hali ya uvimbe kwenye tezi na hata kupunguza uvimbe wa kawaida ambao umetokea ndani ya mwili na pia humsaidia sana mtu akiwa amefanyiwa upasuaji.

Mananasi husaidia mmeng’enyo wa chakula

Mananasi yana virutubisho vya kambakamba (fibre) ambavyo husaidia sana kwenye usagaji wa chakula mwilini. Kirutubisho cha Bromelain pia husaidia kusaga chakula tumboni kwa kuvunja vile vipande vya protini.

Manufaa ya nanasi kwenye ngozi

Vitamini C ipatikanayo kwenye mananasi husaidia kuipa ngozi mng’ao. Pia mishipa midogo ya damu hufaidika kutokana na mananasi pamoja na viungo vingine vya mwili na mifupa pia.

Manufaa ya nanasi kwenye mifupa

Mananasi yana madini aina ya Manganese ambayo husaidia kuzalisha nishati mwilini huku yakisaidia kutoa ulinzi kwa seli za mwili wa mwanadamu.

Madini haya yanasaidia ufanyaji kazi wa madini mengine na virutbisho kama Thiamine na Biotin ambavyo kazi yake kubwa ni kusaidia kufanya mifupa kuwa migumu na yenye afya zaidi na pia husaidia kuyeyusha vyakula vyenye mafuta.

Mananasi husaidia macho

Tunda aina ya nanasi lina vitamin A pamoja na kirutubisho aina ya Beta-Carotene ambavyo kwa pamoja husaidia mfumo wa kinga ya mwili na afya ya macho.

Mananasi hutoa nguvu na nishati na kushusha shinikizo la damu.

Mananasi yana kiwango kikubwa cha Vitamini B1 na B6 na ni vyanzo muhimu sana vya nishati pamoja na kuvunjavunja sukari kwenye mfumo wa usagaji wa chakula.

Madini ya shaba yanayopatikana kwenye mananasi yanasaidia kutoa afya kwa seli nyekundu zinazosaidia kutengeneza damu na madini ya potasia ambayo yanasaidia kuweka mapigo ya moyo sawa na kushusha shinikizo la damu.