MakalaMichezo

Liverpool bila mchezaji kutoka Ufaransa inaweza kutwaa EPL?

March 1st, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TAKWIMU ya ajabu japo ‘ndogo’ inaonyesha viongozi Liverpool hawatashinda Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu wa 2018-2019.

Tovuti ya SPORTbible inasema iwapo vijana wa Jurgen Klopp watatwaa ubingwa, basi watalazimika kuenda kinyume na historia.

“Si kwa sababu ni miaka 29 tangu wanyakue taji la mwisho la ligi, bali pia kwa sababu ya takwimu ya ajabu ya washindi wa Ligi Kuu ya Uingereza katika karne hii ya 21,” tovuti hiyo imesema Jumatatu.

Ushindi wa Liverpool wa mabao 5-0 dhidi ya Watford Jumatano unawaweka katika nafasi nzuri ya kushinda vita hivi vya ligi. Unafanya vijana wa Jurgen Klopp kusalia kileleni kwa alama 69, pointi moja mbele ya mabingwa watetezi Manchester City ambao walinyuka West Ham 1-0.

“The Reds”, jinsi Liverpool inafahamika kwa jina la utani, itashinda ligi timu zote mbili zikishinda mechi zao 10 zilizobaki.

“Liverpool inafahamu kwamba nyuma yake kuna City ambayo inasubiri kuadhibu kosa lolote itafanya kwa sababu vijana wa kocha Pep Guardiola wanawakaribia kabisa,” tovuti hiyo inasema.

Tangu Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ianzishwe, Liverpool imefaulu kuimaliza katika nafasi ya pili mara tatu (2001–2002, 2008–2009 na 2013–2014) kwa hivyo watahitajika kuandika historia upya ili kunyakua taji.

Si historia yao pekee wanahitaji kuandika. Kwa mujibu wa tovuti ya SPORTbible, kila timu iliowahi kuibuka bingwa wa Uingereza katika karne ya 21 imekuwa na Mfaransa kikosini, na Liverpool haina Mfaransa hata mmoja.

Msimu 1999-2000, Mikael Silvestre alibeba taji akisakatia Manchester United na pia kupata ufanisi huo msimu 20002001, 2002-2003 na 2006-2007.

Arsenal iliojaa wachezaji kutoka Ufaransa wakiwemo Thierry Henry, Patrick Vieira, Gilles Grimandi, Robert Pires na Sylvain Wiltord chini ya kocha Arsene Wenger, iliibuka mshindi msimu 2001-2002.

Mohamed Salah wa Liverpool audhibiti mpira klabu yake ilipokabiliana na Watford Februari 27, 2019, uwanjani Anfield ambapo wenyeji Liverpool walishinda 5-0. Picha/ AFP

Wachezaji hawa wote isipokuwa Grimandi walipata ufanisi huo tena katika msimu 2003-2004 ambao Arsenal ilinyakua taji bila kushindwa. Ilikuwa pia imeajiri Wafaransa Jermaine Aliadiere, Pascal Cygan na Gael Clichy.

Clichy kisha alishinda ligi akichezea Manchester City msimu 2011-2012 na 2013-2014 akiwa na Samir Nasri.

Timu ya Manchester United ya msimu 2001-2002 pia ilijumuisha Fabian Barthez na Silvestre na Laurent Blanc msimu 2002-2003. William Gallas na Claude Makelele walikuwa muhimu katika ushindi wa Chelsea misimu 2004-2005 na 2005-2006 chini ya Jose Mourinho.

Louis Saha na Patrice Evra walisaidia United kutamba ligini msimu 2006-2007 na pia 2007-2008, huku Evra pia akiwa katika kikosi kilichosaidia Sir Alex Ferguson kuhifadhi taji msimu 2008-2009.

Nicolas Anelka, ambaye alishinda EPL akisakatia Arsenal kabla ya karne hii, na Florent Malouda, walikuwa katika kikosi cha Chelsea kilichoibuka namba wani msimu 2009-2010. Evra alishinda taji hili tena akiwa United msimu 2010-2011 na tena taji la mwisho la Fergie msimu 2012-2013.

Loic Remy na Kurt Zouma waliibukwa mabingwa wakiwa Chelsea msimu 2014-2015 naye Zuma akashinda 2016-2017 akiwa Stamford Bridge chini ya Antonio Conte.

Katika ushindi wa pili wa Zouma, alikuwa katika kikosi kimoja na N’Golo Kante, ambaye aliongoza Leicester City kuduwaza washiriki wote wa EPL msimu 2015-2016.

Hatimaye, msimu uliopita wa 2017-2018, Aymeric Laporte na Benjamin Mendy walishinda taji na Machester City na hata Equilam Mangala aliwacha Everton, alikokuwa kwa mkopo, ili kufika uwanjani Etihad kupokea medali yake ya washindi.

Kwa hivyo, mara ya mwisho mabingwa wa Uingereza hawakuwa na Mfaransa kikosini ni wakati Manchester United ilishinda mataji matatu msimu 1998-1999.

Swali ni je, Liverpool, ambayo inajivunia wachezaji wakali kama Mohamed Salah (Misri), Sadio Mane (Senegal), Virgil van Dijk (Uholanzi) na Roberto Firmino (Brazil), miongoni mwa mastaa wengine, ina pumzi ya kutosha kuandikisha historia mpya ya kutwaa taji bila mchezaji kutoka Ufaransa? Muda ndio utakuwa msema kweli, ingawa takwimu hizi zinasema kivingine.