Liverpool guu moja ndani ya 4-bora UEFA baada ya kutandika Benfica katika raundi ya kwanza ya robo-fainali ugenini

Liverpool guu moja ndani ya 4-bora UEFA baada ya kutandika Benfica katika raundi ya kwanza ya robo-fainali ugenini

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walitia guu moja ndani ya nusu-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kukomoa Benfica ya Ureno 3-1 katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali mnamo Jumanne usiku jijini Lisbon.

Licha ya ushindi huo, kocha Jurgen Klopp ametaka kikosi chake kutolegeza kamba watakaposhuka dimbani kwa ajili ya marudiano mnamo Aprili 13, 2022 uwanjani Anfield.

Ibrahima Konate aliwaweka Liverpool kifua mbele katika dakika ya 17 kabla ya Sadio Mane kupachika wavuni goli la pili kunako dakika ya 34. Ingawa Darwin Nunez alirejesha Benfica mchezoni mwanzoni mwa kipindi cha pili, Luis Diaz alizamisha kabisa chombo chao katika dakika ya 87 baada ya kumwacha hoi kipa Odysseas Vlachodimos.

“Kuja Lisbon na kushinda Benfica mbele ya mashabiki wao wa nyumbani si kibarua chepesi. Benfica walijitahidi zaidi lakini bahati haikusimama nao. Bado tuna kibarua kigumu katika mkondo wa pili,” akasema Klopp.

Ushindi wa Liverpool uliweka hai matumaini yao ya kujitwalia mataji manne msimu huu. Kabla ya kurudiana na Atletico, kikosi hicho kinachoshikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kitakuwa kimevaana na mabingwa watetezi Manchester City katika ligi ugani Etihad kisha kumenyana tena kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley.

Masogora wa Klopp tayari wamejizolea taji la Carabao Cup msimu huu baada ya kupepeta Chelsea kwa penalti 11-10 mwishoni mwa Februari 2022.

Liverpool walizima Inter Milan 2-1 katika hatua ya 16-bora huku Benfica wakitandika Ajax ya Uholanzi 3-2 katika raundi ya muondoano. Benfica hawajawahi kusonga zaidi ya hatua ya nane-bora katika historia ya UEFA na Bayern Munich iliwaondoa kwenye robo-fainali za 2015-16.

Liverpool walishuka dimbani dhidi ya Benfica baada ya kucharaza Watford 2-0 katika EPL mnamo Aprili 2, 2022. Mechi ya UEFA iliyoshuhudia Inter ikiwachapa Liverpool 1-0 ugani Anfield mnamo Machi 8, ndiyo ya pekee ambayo masogora hao wa kocha Klopp wamepoteza kati ya 18 zilizopita katika mashindano yote.

Liverpool sasa wameshinda mechi zote saba zilizopita ugenini huku wapinzani wakikosi kuwafunga kwenye michuano yote ya ugenini mnamo Februari na Machi 2022. Liverpool walibanduliwa na Real Madrid kwa mabao 3-1 kwenye robo-fainali za UEFA mnamo 2020-21 huku Benfica ikiwadengua kwa magoli 3-0 kwenye hatua ya 16-bora mnamo 2005-06.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi mtaa wa mabanda wakiuka hali ngumu na kufanya...

ODM: Waliofaulu mchujo kaunti 2

T L