Michezo

Liverpool hawakamatiki baada ya kuitia adabu Arsenal

December 31st, 2018 2 min read

NA MASHIRIKA

MERSEYSIDE, UINGEREZA

LIVERPOOL walifungua pengo kubwa la alama kileleni mwa jedwali na kuanika azma ya kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kuwadhalilisha Arsenal 5-1 ugani Anfield mnamo Jumamosi.

Licha ya Arsenal kuwekwa kifua mbele kupitia kwa bao la Ainsley Maitland-Niles kunako dakika ya 11, Liverpool walirejeshwa mchezoni na nyota Roberto Firmino aliyepachika wavuni jumla ya mabao matatu.

Magoli mengine ya Liverpool ambao wanashuhudia ufufuo mkubwa chini ya kocha Jurgen Klopp yalipachikwa wavuni kupitia kwa wavamizi Sadio Mane na Mohamed Salah.

Kufikia sasa, Liverpool wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 54, tisa zaidi kuliko Tottenham Hotspur ambao pia waliduwazwa na limbukeni Wolverhampton Wanderes waliowapokeza kichapo cha 3-1 ugani Wembley.

Kushindwa kwa Arsenal kuliwasaza katika nafasi ya tano jedwalini kwa alama 38, jambo ambalo linawaweka katika hatari ya kupitwa na Manchester United ambao jana walikuwa wenyeji wa Bournemouth uwanjani Old Trafford.

Ushirikiano mkubwa kati ya Firmino, Salah na Mane uligeuka kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Arsenal ambayo ilikuwa chini ya udhibiti wa Sokratis Papastathopoulos, Stephan Lichtsteiner, Sead Kolasinac na Shkodran Mustafi aliyeondolewa ugani katika kipindi cha pili na nafasi yake kutwaliwa na Laurent Koscielny.

Kwa mujibu wa Klopp, ushindi wao dhidi ya Arsenal unatarajiwa kuwa kiini cha hamasa yao wanapojiandaa kwa sasa kuvaana na mabingwa watetezi Man-City katika mchuano mwingine wa haiba kubwa utakaosakatwa ugani Etihad mwishoni mwa wiki hii.

Wakijipa malengo mapya katika kampeni za muhula huu, beki Dejan Lovren wa Liverpool amefichua kwamba klabu hiyo kwa sasa inapania kunyanyua ufalme wa EPL bila ya kupoteza hata mchuano mmoja.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa ushindi huu mkubwa. Nimefurahi kwa sababu Tottenham ambao pia ni wapinzani wetu wakuu, walishindwa. Sisemi lolote kuhusu hali ya kusuasua kwa Man-City ambao wamepoteza michuano mitatu ligini kati ya minne iliyopita,” akatanguliza Klopp.

“Kila timu ingali vitani. Kosa kubwa litakalofanywa na Liverpool ni kuanza kuwabeza wapinzani au kulegeza kamba. Hatuwezi kabisa kupuuza kikosi chochote kilichopo ndani ya mduara wa sita-bora kwa sasa,” akaongeza Klopp.

Kulingana na kocha huyo mzawa wa Ujerumani, ukubwa wa viwango vya ushindani katika kampeni za EPL msimu huu huenda ukafanya mshindi wa EPL kuamuliwa katika majuma ya mwisho.

Kwa upande wake, kocha Unai Emery wa Arsenal alisema Liverpool wanajivunia kikosi imara kilicho na uwezo wa kutwaa ubingwa msimu huu. Aidha, alikiri kwamba uwepo wa Mane, Firmino na Salah kambini mwa Klopp ni sifa inayofanya Liverpool kuwa miongoni mwa klabu zenye safu bora zaidi za uvamizi.

“Wana kikosi imara ambacho kilijisuka vilivyo katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji. Wanajivunia uthabiti katika takriban kila idara. Hii ni sifa ya kikosi ambacho kinatawaliwa na kiu ya kunyanyua mataji ya haiba kubwa,” akasema Emery kwa kudokeza uwezekano wa Arsenal kujitoma sokoni mnamo Januari 2019 na kusajili mabeki wa viwango vya juu.

“Ukitaka kutwaa mataji katika kampeni zozote, ni lazima usajili matokeo mazuri. Bila shaka Liverpool wamedhihirisha kwamba wana huo uwezo,” akaongeza.

Katika misimu minane kati ya 10 iliyopita, klabu ambayo imekuwa ikiongoza jedwali la EPL baada ya kupigwa kwa nusu ya michuano yote kufikia wakati wa Krismasi imekuwa ikitwaa ubingwa.

Hata hivyo, Liverpool iliwahi kuongoza mara mbili kufikia wakati kama huo mnamo 2008-09 na 2013-14 kabla ya kupitwa na kuambulia nafasi ya pili mwishowe.

Hili ni jambo ambalo Klopp amepania kulirekebisha muhula huu kambini mwa Liverpool ambao hawajapoteza mechi yoyote kati ya 20 iliyopita katika EPL.