Liverpool hawatasajili mchezaji yeyote muhula huu wa Januari 2021 – Klopp

Liverpool hawatasajili mchezaji yeyote muhula huu wa Januari 2021 – Klopp

Na MASHIRIKA

LICHA ya Liverpool kukosa huduma za mabeki tegemeo Virgil van Dijk na Joe Gomez kwa muda mrefu katika kampeni za msimu huu, kocha Jurgen Klopp amesisitiza kwamba mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hawatasajili sogora yeyote mwezi huu wa Januari.

Kwa mujibu wa Klopp, hazina ya Liverpool kifedha imetikiswa pakubwa na Covid-19 kiasi kwamba watalazimika kutegemea wanasoka waliopo kwa sasa kambini.

“Huenda kuna baadhi ya klabu ambazo hazina changamoto tele za kifedha. Lakini Liverpool wameathiriwa na huo ndio msimamo wa klabu pamoja na wasimamizi,” akasema Klopp.

Licha ya kukosa maarifa ya mabeki wao wa haiba kubwa, Liverpool wangali kileleni mwa jedwali la EPL japo wamekuwa wakisuasua pakubwa katika kipindi cha majuma machache yaliyopita yaliyowashuhudia wakijizolea alama mbili pekee kutokana na mechi tatu zilizopita.

“Ingawa ni matamanio ya kila kocha kujishughulisha sokoni na kutafuta mwanasoka atakayebadilisha matokeo ya kikosi, sioni uwezekano wowote wa kusajiliwa kwa mchezaji mpya uwanjani Anfield mwezi huu wa Januari,” akasema kocha huyo raia wa Ujerumani.

“Tumeshinda taji la EPL, tukanyakua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Kombe la Dunia. Kikosi kilikuwa katika hali shwari kabisa katika vipindi vyote vya ushindi huo. Lakini hali kwa sasa ni tofauti kabisa kwa kuwa mabeki watatu tegemeo wana majeraha. Kikawaida huu ndio wakati wa kutafuta nguvu mpya sokoni ila Liverpool hawana mpango huo,” akasema Klopp.

Kuumia kwa Van Dijk, Joel Matip na Gomez mwanzoni mwa msimu huu kulimweka Klopp katika ulazima wa kuanza kutegemea huduma za wachezaji chipukizi Rhys Williams na Nathaniel Phillips walioshirikiana vilivyo na Fabinho pamoja na nahodha Jordan Henderson.

Liverpool kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 33 sawa na Manchester United ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na mabingwa hao watetezi.

You can share this post!

AKILIMALI: Ufugaji wa mbuzi wa maziwa una faida, mfugaji...

Malkia Strikers kupiga kambi ya mazoezi bara Asia au Ulaya...