Michezo

Liverpool imani tele itatwaa ufalme Uingereza

April 24th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, Uingereza

LIVERPOOL wanaendelea kudhibiti uongozi wa msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa pointi 88 mbele ya Manchester City kwa tofauti ya pointi moja, lakini City watarejea kileleni iwapo watafanikiwa kuwabwaga Manchester United leo Jumatano usiku ugani Old Trafford.

Manchester wamebakiza mechi nne huku Liverpool ikibakia na tatu, lakini zote zina uwezo wa kumaliza msimu kwa zaidi ya pointi 90.

Baada ya kuvaana na Man-United, City watakutana na Burnley, Leicester City halafu Brighton. Liverpool nayo ina kazi ya kutimiza mbele ya Huddersfield, Newcastle United na mwishowe Wolves.

Nafasi ya tatu inamilikiwa na Tottenham Hotspur iliyo na pointi 67, sawa na Chelsea wanaokamata nafasi ya nne, mbele ya Arsenal walio na pointi 66, lakini Chelsea wamecheza mechi 35, wakati Arsenal wakifikisha mechi 34.

Man-United ilijiharibia yenyewe kuwa katika mduara wa nne-bora baada ya kupokea kichapo cha 4-0 dhidi ya Everton, kukamilisha mechi tano mfululizo walizopoteza wakiwa katika uwanja wa ugenini baada ya hapo awali kushindwa na Arsenal, Wolves (mara mbili) na miamba wa soka ya Uhispania, Barcelona.

Tangu timu hiyo imwajiri Sir Alex Ferguson mnamo 1986, ilikuwa haijawahi kupoteza mechi tano mfululizo za ugenini ndani ya msimu mmoja.

Kichapo hicho cha mabao mengi zaidi tangu kocha Ole Gunnar Solskjaer apewe kazi ya mkataba wa miaka mitatu, kimekuja wakati timu hiyo imeanza kupata matokeo yasiyoridhisha ambayo yamerudisha kumbukumbu za awali chini ya kocha Jose Mourinho.

Spurs, Chelsea na Arsenal zote zimetinga nusu-fainali ya michuano ya kuwania ubingwa wa Ulaya, hapa kukiwa na uwezekano wa timu tano za EPL kufuzu kwa michuano ya UEFA msimu ujao.

Kwa mfano, iwapo Spurs na Chelsea zitashinda mataji ya UEFA na Ligi ya Europa mtawalia, na kumaliza ligi katika nafasi za tano na sita, timu itakayomaliza katika nafasi ya nne ligini itashuka na kucheza mechi za Europa League.

Ratibani, Spurs watacheza na Brighton, West Ham United, Bournemouth na baadaye Everton.

Arsenal itakutana na Wolves, Leicester City, Brighton na baadaye Burnley, wakati Chelsea wakipambana na Man-United, Watford na mabingwa wa zamani, Leicester City.

Mshahara

Wakati uo huo, kiwango cha mshahara anachokitaka kiungo wa Man-United Paul Pogba, 26, kinaweza kikawa kikwazo kwa Real Madrid kumsajili nyota huyo raia wa Ufaransa.

Man-United ipo tayari kumpandisha Mike Phelan mpaka kuwa mkurugenzi wa ufundi, na nafasi yake ya meneja msaidizi kupewa kiongozi wa zamani wa klabu hiyo, Michael Carrick.