Michezo

Liverpool ina nafasi kutinga fainali UEFA, Daglish asema

May 7th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

NYOTA wa zamani wa Liverpool Kenny Daglish ameeleza matumaini yake kwamba timu hiyo ina uwezo wa kuyafunga mabao matatu na kuibandua Barcelona kwenye kipute cha Klabu Bingwa Barani Ulaya(UEFA) Jumanne Mei 7 ugani Anfield.

“Nafikiri Liverpool bado wana nafasi ya kufika fainali kwenye UEFA ingawa bado wa mlima wa kuukwea dhidi ya Barcelona. Nitakuwa mjinga iwapo nitasema hawana nafasi kabisa ila lazima wamchunge Lionel Messi ambaye anaweza kuzamisha chombo chao zaidi wakilegea,” akasema Daglish ambaye pia aliwahi kuinoa The Reds.

“Ugani Camp Nou, kikosi cha Liverpool kilicheza vizuri na hata kuizidi Barcelona maarifa na iwapo wataendeleza mchezo huo mbele ya mashabiki wa nyumbani, nina hakika watatamba na kuwashangaza wengi,” akaongeza Daglish.

Liverpool wataingia kwenye mchuano huo wakilenga kurejesha kumbukumbu ya mwaka 2005, walipotoka nyuma baada ya kufungwa mabao matatu na AC Milan ya Italia kisha kuyarejesha mabao hayo katika kipindi cha pili na kushinda ubingwa wa UEFA mwaka huo kupitia mikwaju ya penalti.

Hata hivyo, Liverpool wataweza kuyageuza matokeo hayo nyumbani iwapo watawathibiti Messi na Luis Suarez ambao ushirikiano wao umeiwezesha Barcelona kutwaa ubingwa wa Laliga huku wakionyesha ghera ya kutia kapuni taji la UEFA pia.

Messi alifunga mabao mawili katika mkondo wa kwanza na yupo njiani kutwaa taji la mchezaji bora duniani maarufu kama Ballon d’Or hasa baada ya kufikisha idadi ya mabao hadi 600 tangu anze kuchezea Barcelona wiki hii.