Michezo

Liverpool ina uwezo wa kushinda EPL na UEFA – Henderson

February 19th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

NAHODHA wa Liverpool Jordan Henderson anaamini kwamba klabu hiyo inaweza kuhimili ushindani mkali na kutwaa mataji ya Klabu Bingwa Barani Uropa (UEFA) na Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Liverpool inafukuzia ubingwa wa EPL wakati inakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Manchester City na Tottenham Hot Spurs. Kwa upande mwingine vijana wa Jurgen Klopp wanakibarua kigumu dhidi ya Bayern Munich kwenye hatua ya mwoondoano ya kipute cha UEFA, mkondo wa kwanza ukigaragazwa ugani Anfield Jumanne Februari 19.

Hata hivyo, Henderson anaamini kwamba kikosi cha sasa cha Liverpool kinajivunia wachezaji mahiri wanaoweza kuhimili presha zinazotokana na ushindani katika mashindano hayo mawili na hatimaye kushinda mataji hayo.

“Iwapo tungekuwa na hiari basi tungechagua kushinda ligi pamoja na UEFA. Hata hivyo vipute vyote viwili vina umuhimu mkubwa kwetu na mchuano wa Jumanne ni mechi kubwa zaidi kwa kikosi cha Liverpool msimu huu,”

“Nina imani kwamba kikosi cha sasa ni dhabiti na kinaweza kushinda mashindano yote mawili. Iwapo hilo litakosa kutimia basi lazima tushinde moja kati ya mataji ya UEFA na EPL,” akasema Henderson akizungumzia mechi dhidi ya Bayern Munich.

Ingawa hivyo, vijana hao wa Anfield wanapigiwa upato kutamba na kufuzu robo fainali baada ya Bayern kuendelea kusuasua msimu wa 2018/19 katika ligi yao ya nyumbani (Bundesliga) tangu wamteue Niko Kova? kama kocha wao.

Bayen Munich wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Bundesliga, alama mbili nyuma ya viongozi Borussia Dortmund. Ijumaa Februari 16, vijana wa kocha Kovac walilazimika kutoka nyuma na kushinda Augsburg 3-2.