Liverpool kuipa Manchester City taji ikipigwa leo

Liverpool kuipa Manchester City taji ikipigwa leo

LIVERPOOL watavaana na Southampton leo Jumanne ugani St Mary’s katika pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambalo wana ulazima wa kushinda ili kuchelewesha zaidi karamu ya Manchester City wanaopigiwa upatu wa kuhifadhi taji la kipute hicho.

Huku ushindi kwa Liverpool ukidumisha uhai wa matumaini yao ya kujizolea makombe manne muhula huu, kichapo kitavunia Man-City taji la sita la EPL na la nne chini ya kocha Pep Guardiola.

Hakuna klabu katika historia ya soka ya Uingereza imewahi kunyanyua mataji manne kwenye kampeni za msimu mmoja.

Southampton wamekuwa na siku 10 za kujifua kwa kipute cha leo Jumanne tangu Brentford wawapepete 3-0 ugenini.

Kwa upande wao, Liverpool watashuka dimbani wakijivunia motisha tele baada ya kukomoa Chelsea kwa penalti 6-5 na kunyanyua Kombe la FA kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16.

Taji hilo lilikuwa la nane kwa Liverpool katika FA Cup na la pili katika kampeni za muhula huu. Walitandika Chelsea kwa penalti 11-10 mwishoni mwa Februari na kutwaa ubingwa wa Carabao Cup.

Ushindi dhidi ya Southampton na Wolves katika mechi mbili zijazo za EPL utawachochea kulipiza kisasi dhidi ya Real Madrid kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 28 jijini Paris, Ufaransa.

Kufikia sasa, Liverpool wanakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 86, nne nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi Man-City ambao wametandaza mchuano mmoja zaidi.

Man-City wangejipa asilimia kubwa ya uhakika wa kutwaa taji la EPL iwapo wangepiga West Ham United jijini London mnamo Jumapili.

Hata hivyo, waliambulia sare ya 2-2 katika gozi hilo. Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool watatia kibindoni taji la EPL msimu huu – la 20 katika historia – iwapo watashinda mechi mbili zilizosalia nao Man-City wapoteze au waambulie sare dhidi ya Aston Villa ugani Etihad mnamo Mei 22.

Southampton wameshinda pambano moja pekee kati ya 11 yaliyopita katika EPL.

Matokeo hayo yamewasaza katika nafasi ya 15 jedwalini kwa alama 40 zinazowapa uhakika wa kusalia ligini muhula ujao.

Liverpool walitandika Villa 2-1 katika mchuano uliopita ligini. Ushindi huo ulikuwa wao wa saba kutokana na mechi nane mfululizo za EPL ugenini.

Hata hivyo, uthabti wao umetikiswa na majeraha yatakayowaweka nje masogora Fabinho Tavares, Mohamed Salah na Virgil van Dijk.

Japo Southampton waliduwaza Liverpool kwa kichapo cha 1-0 ugani St Mary’s msimu jana, masogora wa Klopp walilipiza kisasi kwa kuvuna ushindi wa 4-0 katika mkondo wa kwanza wa EPL muhula huu uwanjani Anfield.

  • Tags

You can share this post!

Umuhimu wa kuosha miguu usiku kwa maji ya moto

CHARLES WASONGA: Ni picha mbaya Sonko kushambuliwa katika...

T L