Michezo

Liverpool kujinyanyua dhidi ya Salzburg UEFA

October 2nd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MERSYSIDE, Uingereza

WAFALME wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) Liverpool wanaialika Red Bull Salzburg ya Austriakwa mara ya kwanza uwanjani Anfield leo Jumatano usiku.

Wenyeji watakuwa wakipigania ushindi wa kwanza msimu huu katika michuano hiyo baada ya kubwagwa 2-0 na Napoli katika pambano la ufunguzi la Kundi E, siku ambayo Red Bull Salzburg waliibuka na ushindi mkubwa wa 6-2 dhidi ya Genk kutoka Ubelgiji. Lakini baada ya kufika fainalini mara mbili na kushinda ubingwa mwezi Juni, hii ikiwa mara yao ya sita, Liverpool wamethibitisha ushupavu wao.

Kichapo cha 2-0 mikononi mwa Napoli ugani San Paolo kilipotosha mawazo ya mashabiki kwa kiasi fulani, lakini itakumbukwa kwamba hiyo ilikuwa tu mechi ya kwanza kundini.

Haikukuwa mara ya kwanza kwa Liverpool kushindwa ugenini katika kiwango, hiki, lakini mbele ya mashabiki wao wa nyumbani, ‘The Reds’ wanatarajiwa kuwa moto wa kuotea mbali ugani Anfield ikikumbukwa mwenendo wao mzuri katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Msimu uliopita, vijana hao wa kocha Jurgen Klopp walichapwa mara tatu ugenini, lakini wakasonga mbele na kutwaa ubingwa kwa kuwatandika Tottenham.

Matokeo yao mazuri ya majuzi yalitokea dhidi ya Barcelona waliponyuka mabingwa hao wa Uhispania 4-0 katika nusu-fainali. Wenyeji wanaingia uwanjani baada ya ushindi wa majuzi wa 1-0 dhidi ya Shefield United waliowatoa jasho jingi katika EPL.

Baada ya mechi ya leo Jumatano, Liverpool watarejea uwanjani Jumamosi kucheza na Leicester City kabla ya mechi nyinginezo kubwa dhidi ya Manchester United, Genk, Tottenham Hotspur na baadaye Arsenal.

Lakini kwa sasa, kila mtu pale Anfield anaangazia mechi ya leo usiku, ikikumbukwa kwamba watakuwa wakicheza na timu ambayo iliandikisha ushindi mkubwa dhidi ya Genk.

Ushindi wa Salzburg unadhihirisha uhodari wa washambuliaji wao ambao kufikia sasa msimu huu, tayari wamepachika wavuni mabao 55 katika mechi 12 za mashindano tofauti.

Kinda Erling Haaland mwenye umri wa miaka 19 amekuwa ndiye matata zaidi kwenye safu hiyo ya ushambuliaji, akijivunia mabao 17, mbali na kutoa pasi kadhaa zilizosababisha mabao.

Msimu huu, amefunga ‘hat-trick’ nne, moja ikitokea kwenye mechi yao dhidi ya Genk, lakini huenda asicheze leo Jumatano kutokana na jeraha linalomsumbua.

Ratiba ya mech za leo usikukwa ufupi ni: Slavia Praha na Borussia Dormund; Genk na Napoli; Liverpool na Red Bull Sulzbury; LOSC na Chelsea; Zenit na Benfica, Valencia na Ajax Amsterdam; Barcelona na Inter Milan halafu RB Leipzig na Lyon.