Michezo

Liverpool kutwaa huduma za Thiago kipindi cha lala salama

September 15th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA 

LIVERPOOL watasubiri hadi dakika za mwisho katika muhula huu wa uhamisho wa wachezaji ili kumsajili kiungo matata raia wa Uhispania, Thiago Alcantara kutoka Bayern Munich ya Ujerumani.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndio wanapigiwa upatu wa kumtwaa Alcantara ambaye pia anawaniwa na Manchester United na Arsenal.

Man-United wamemfikia wakala wa Alcantara kuulizia uwezekano wa kumsajili kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29 ila huenda wasiwe tena na pupa ya kumtwaa baada ya kuja kwa Donny van de Beek kutoka Ajax ya Uholanzi.

Kwingineko, kusajiliwa kwa Willian Borges na matokeo bora ya Mbrazil huyo katika mechi yake ya kwanza ndani ya jezi za Arsenal huenda kukapunguza kasi ya kocha Mikel Arteta kutaka kumsajili Alcantara.

Vita vya Chelsea kuwania pia huduma za Declan Rice na Wilfried Zaha wa Crystal Palace huenda vikaamuliwa na hatima ya chipukizi Jadon Sancho anayehusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Old Trafford kuvalia jezi za Man-United.

“Iwapo Barcelona watamsajili Georginio Wijnaldum kutoka Liverpool, basi kocha Jurgen Klopp atakuwa na ulazima wa kumsajili Alcantara ili awe kizibo cha kiungo huyo raia wa Uholanzi,” akasema wakala wa Alcantara.

“Liverpool wangekuwa tayari wamejinasia huduma za sogora huyo iwapo wangeweka mezani kima cha Sh3.4 bilioni zinazotakiwa na Bayern,” akaongeza.

Liverpool tayari wamemsajili kipa chipukizi Marcelo Pitaluga, 17, kutoka Fluminense kwa kima cha Sh980 milioni.

Mnamo Septemba 13, 2020, Zaha ambaye ni raia wa Ivory Coast, aliwataka Palace wamwachilie ili ajiunge na Chelsea au Everton.

Kocha Roy Hodgson wa Palace amethibitisha kwamba nyota huyo wa zamani wa Manchester United tayari amewasilisha ombi la kuruhusiwa kubanduka ugani Selhurst Park kufikia Oktoba 5, 2020 ambayo ni siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji.

Zaha, 27, alifunga bao la pekee lililowasaidia Palace kuwalaza Southampton 1-0 katika mchuano wao wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Hadi kufikia mwisho wa msimu uliopita wa 2019-20, Zaha alikuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa w akusajiliwa na Arsenal ambao badala yake walishawishika kumtwaa nyota Nicolas Pepe wa Ivory Coast.

Kushindikana kwa uhamisho wa Zaha hadi Arsenal ni jambo ambalo kocha Hodgson alisema kwamba liliathiri pakubwa matokeo ya mchezaji huyo msimu uliopita wa 2019-20.

“Zaha hajatulia tangu uhamisho hadi Arsenal utibuke. Hata hivyo, tunajitahidi kumsadikisha aendelee kuwa mchezaji wetu. Tusubiri tuone yatakayotokea kati ya sasa na Oktoba 5,” akasema Hodgson ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO