Michezo

Liverpool kuvaana na Arsenal huku Spurs wakionana na Chelsea raundi ya 16-bora ya Carabao Cup

September 25th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MIAMBA wa soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool, watakutana sasa na Arsenal kwenye raundi ya 16-bora ya kipute cha Carabao Cup mnamo Oktoba 1, 2020 baada ya kuwakomoa Lincoln 7-2 uwanjani Sincil Bank mnamo Alhamisi.

Arsenal ya kocha Mikel Arteta, ilifuzu kwa hatua ya 16-bora baada ya kuzamisha chombo cha Leicester City kwa mabao 2-0 mnamo Septemba 23 uwanjani King Power.

Wakicheza dhidi ya Lincoln, Liverpool ambao kwa sasa wananolewa na kocha Jurgen Klopp, walifungiwa mabao yao na Takumi Minamino, Curtis Jones, Xherdan Shaqiri, Marko Grujic na Divock Origi.

Tottenham Hotspur walifuzu kwa hatua ya 16-bora bila ya kutoa jasho baada ya kupokezwa tiketi ya bwerere. Hatua hiyo ilichangiwa na tukio la idadi kubwa ya wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Leyton Orient waliokuwa wavaane na Spurs kuugua Covid-19. Spurs ya mkufunzi Jose Mourinho sasa itachuana na Chelsea ya kocha Frank Lampard.

Chini ya kocha Pep Guardiola, waliwapepeta Bournemouth 2-1 na kujikatia tiketi ya kuvaana na Burnley katika raundi ijayo ya 16-bora.

Kati ya mechi nyinginezo zilizotandazwa Septemba 24, Aston Villa walisajili ushindi wa 3-0 dhidi ya Bristol City ugani Ashton Gate na kufuzu kumenyana na Stoke City kwenye gozi litakaloshuhudia mshindi akitinga hatua ya robo-fainali ya Carabao Cup msimu huu.

DROO YA 16-BORA CARABAO CUP:

Tottenham na Chelsea

Newport County na Newcastle

Burnley na Man-City

Brighton na Man-United

Everton na West Ham

Brentford na Fulham

Aston Villa na Stoke City

Liverpool na Arsenal