Michezo

Liverpool kuwatema Origi, Shaqiri, Keita, Lallana, Lovren, Grujic na Wilson

June 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Jurgen Klopp anatarajiwa kuwatema wanasoka sita wa kikosi cha kwanza kadri anavyopania kutafuta fedha za kujinasia huduma za masogora anaowamezea mate katika muhula ujao wa uhamisho wa wachezaji.

Liverpool wamekuwa wakiyahemea maarifa ya wanasoka wawili wa Wolves – Ruben Neves na Adama Traore ambao thamani yao inakisiwa kufikia jumla ya Sh15.4 bilioni.

Neves ambaye ni kiungo matata wa Ureno hatakuwa radhi kuondoka uwanjani Molineux bila Sh7 bilioni huku Mhispania Traore akitazamiwa kuachiliwa na kikosi cha kocha Nuno Espirito iwapo Liverpool wataweka mezani kima cha Sh8.4 bilioni.

Klopp anatazamia kuimarisha safu yake ya kati hasa ikizingatiwa kwamba kiungo Georgio ‘Gini’ Wijnaldum angali na mwaka mmoja pekee kwenye mkataba wake na Liverpool wanaotarajiwa kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

Klopp pia anatarajiwa kumtema kiungo mzawa wa Guinea, Naby Keita baada ya kisu cha makali ya kiungo huyo wa zamani wa RB Leipzig aliyegharimu Liverpool Sh7.2 bilioni kusenea.

Keita amewajibishwa na Liverpool mara tisa pekee hadi kufikia sasa msimu huu na huenda akapokezwa msimu mmoja zaidi kuthibitisha ukubwa wa uwezo alionao uwanjani.

Sogora mwingine anayetazamiwa kuondoka Liverpool mwishoni mwa msimu huu ni kiungo mzawa wa Uswisi Xherdan Shaqiri ambaye amekuwa akisugua benchi katika michuano mingi ya msimu huu.

Sogora huyo wa zamani wa Stoke City anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua uwanjani St James’Park kuvalia jezi za Newcastle United.

Nyota mwingine anayetazamiwa kubanduka ugani Anfield ni mshambuliaji Divock Origi ambaye amekosa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Liverpool katika michuano mingi ya haiba kubwa kutokana na ubora wa fomu ya Roberto Firmino wa Brazil.

Beki Dejan Lovren ni mwanasoka mwingine ambaye yuko njia kuondoka uwanjani Anfield kwa pamoja na Marko Grujic na Harry Wilson ambaye kwa sasa huvalia jezi za Bournemouth kwa mkopo.

Adam Lallana tayari anazamiwa kukatiza uhusiano wake na Liverpool baada ya mkataba wake kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu. Mwingereza huyo anahusishwa na uwezekano wa kuungana na Brendan Rodgers kambini mwa Leicester City.