Michezo

Liverpool na Chelsea zajinyanyua Uefa

October 4th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL, Uingereza

TIMU za Liverpool na Chelsea ziliandikisha ushindi wao wa kwanza katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kuchapa Salzburg 4-3 na Lille 2-1 Jumatano, mtawalia.

Liverpool, ambayo ilianza kampeni ya kutetea taji kwa kubwagwa 2-0 na Napoli wiki mbili zilizopita, ilitolewa kijasho chembamba kabla ya kutamba uwanjani Anfield.

Vijana wa Jurgen Klopp waliongoza mchuano huu wa Kundi E kwa mabao 3-0 yaliyopatikana kupitia Sadio Mane dakika ya tisa, Andrew Robertson (25) na Mohamed Salah (36).

Hata hivyo, walitupa uongozi huo waliporuhusu wageni wao kutoka nchini Austria kusawazisha kupitia mabao ya Hwang Hee-chan dakika ya 39, Takumi Minamino (56) na chipikizi matata Erling Braut Haaland (60).

Salah alihakikishia timu yake ushindi dakika tisa baadaye.

“Tulipokuwa tukishinda kwa mabao matatu, tulihitaji kuongeza bao la nne, tano na sita…,” alisema Salah.

Bao la Salah lilikuwa lake la sita msimu huu katika mashindano yote. Limeweka Liverpool bega kwa bega na Salzburg kwa alama tatu, moja nyuma ya viongozi Napoli waliokubali sare ya 0-0 dhidi ya Genk.

Baada ya mechi hiyo, Klopp alisema anaamini mabingwa hao wa Bara Ulaya wanastahili kujikakamua.

“Tulilegea na kuwafungulia milango na wakatusumbua sana,” alisema.

“Ni muhimu kupata mafunzo wakati wa mechi na kuyazungumzia baadaye.

“Lilikuwa funzo muhimu sana kwetu. Nilifahamu hapo awali kuwa tunastahili kuimarika na sasa kila mtu anakubaliana nami.”

Chelsea yafufua kampeni

Mabingwa wa Ligi ya Uropa, Chelsea, ambao pia walikanyagwa 1-0 na Valencia katika mechi ya ufunguzi, walifufua kampeni yao walipozamisha Lille 2-1 katika Kundi H kupitia mabao ya Tammy Abraham na Willian nchini Ufaransa. Abraham aliweka Chelsea bao 1-0 juu dakika ya 22. Victor Osimhen alisawazisha dakika 11 baadaye kabla ya Willian kufunga la ushindi dakika ya 77.

Ajax inaongoza kundi hili kwa alama sita baada ya kunyamazisha wenyeji Valencia 3-0 kupitia mabao ya Hakim Ziyech, Quincy Promes na Donny van de Beek. Mchezaji wa Valencia, Daniel Parejo alipoteza penalti katika kipindi cha kwanza.

Katika mechi zingine zilizosakatwa Jumatano, Achraf Hakimi alifunga bao moja katika kila kipindi Borussia Dortmund ikilima wenyeji Slavia Prague 2-0 katika Kundi F nayo Zenit Saint Petersburg ikalemea Benfica 3-1 nchini Urusi.