Michezo

Liverpool na City zimewapa mashabiki burudani tosha katika kivumbi cha EPL

May 6th, 2019 3 min read

NA ADUNGO OKALIAS 

IMESALIA raundi moja zaidi kwa kivumbi cha kuwania ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kutamatika rasmi.

Tofauti na misimu mingine ya awali, kampeni za muhula huu zimeshuhudia ushindani mkali kati ya klabu mbili za kwanza na nne nyinginezo ambazo zimekuwa zikiwania nafasi mbili za ziada za kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa (UEFA) msimu ujao.

Kubwa zaidi ambalo wakufunzi Pep Guardiola na Jurgen Klopp wamefanikiwa kwalo, ni kuwapa mashabiki wa soka ya EPL burudani tosha na kitu kipya cha kufuatilia zaidi katika msimu ujao wa kipute hicho.

Katika msimu wake wa tatu uwanjani Etihad, Guardiola ambaye ni mzaliwa wa Uhispania amefaulu kuwachochea masogora wake wa Manchester City kupiga soka safi zaidi yenye pasi za uhakika kama walivyokuwa wakicheza Barcelona wakati mkufunzi huyu alipokuwa akidhibiti mikoba ya miamba hao wa soka ya Uhispania.

Chini ya Guardiola, Man-City kwa sasa wamedhihirisha kwamba wana uwezo wa kutandaza soka ya kuvutia katika michuano yote ya haiba kubwa ndani ya Uingereza na kwenye mapambano ya bara Ulaya (UEFA).

Ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba huenda Man-City wakatawazwa mabingwa wa mataji matatu mwishoni mwa kampeni za muhula huu. Mbali na kufukuzia ubingwa wa EPL ambao wana kiu kubwa ya kutetea, Man-City wanapigiwa upatu wa kuwapepeta Watford mwishoni mwa mwezi huu na kunyanyua ufalme wa Kombe la FA.

Leo, Man-City wameratibiwa kuvaana na mabingwa wa EPL 2015-16, Leicester City uwanjani Etihad. Ni mchuano ambao Man-City wana ulazima wa kuvuna ushindi ili kudumisha uhai wa matumaini ya kutawazwa mabingwa wa EPL katika siku ya mwisho ya kampeni za msimu huu. Kwa kweli, hatima ya Man-City katika kivumbi cha EPL muhula huu imo mikononi mwao wenyewe.

Kujikwaa kwao dhidi ya Leicester, ingawa sioni uwezekano wa Man-City kufanya hivyo, kutawatia Liverpool hamasa zaidi ya kuwachabanga Wolves katika siku ya mwisho na kutwaa ubingwa wa taji la EPL. Man-City watafunga kampeni zao za ligi dhidi ya Brighton ugenini.

Mbali na Liverpool, hakuna timu yoyote nyingine katika EPL ambayo kwa sasa inacheza mpira wa kushambulia zaidi kama Man-City ya Guardiola. Tottenham, Chelsea, Arsenal na Manchester City waliokuwa wawe wapinzani wao wakuu, wamekuwa wakisuasua pakubwa.

Ingawa Liverpool wameanika kiu ya kutoa ushindani mkali kwa wapinzani wao hawa wakuu hadi mwisho, vita vya ubabe kati ya Klopp na Guardiola vimechangia sana kukoleza ladha na utamu wa EPL kadri wawili hao wanavyopigania fursa ya kutawala kabisa soka ya Uingereza.

Hadi mwishoni mwa wiki jana, Liverpool na Man-City walikuwa wamebadilishana usukani wa EPL kwa mara 35 tangu kipenga cha kuashiria mwanzo wa msimu huu kipulizwe.

Ingawa timu nyingi zikiwemo Arsenal na PSG zimejaribu sana kuiga mtindo wa kupiga pasi fupi kama ilivyosisitizwa na Guardiola ugani Camp Nou, makocha wa vikosi hivyo bado hawajafanikiwa kabisa kufikia kiwango cha mkufunzi huyo.

Barcelona na Bayern ni miongoni mwa timu ambazo kwa muda mrefu zilitawala sana ulimwengu wa soka ya kisasa kwa jinsi ambavyo usingeweza kabisa kuona katika ligi nyinginezo ikiwemo EPL. Mambo yalianza kubadilika baada ya ujio wa Guardiola aliyetua ugani Etihad katika msimu wa 2016-17.

Katika EPL, klabu nyingi hupania sana kudhihirisha ushindani mkubwa, na hivyo si kawaida kwa timu fulani kufanikiwa kuwatawala wapinzani wake kutoka msimu mmoja hadi mwingine. Ingawa hivyo, Man-City msimu huu wameonyesha mara kwa mara kwamba wana uwezo wa kutamalaki kila mchuano kwa namna ya kipekee na kufunga idadi kubwa ya mabao dhidi ya timu yoyote.

Kufikia sasa, Man-City wamesajili ushindi mara 30, kuambulia sare mara mbili na kupoteza mechi nne kati ya 36 zilizopita ambazo zimewapa mabao 90. Cha kuvutia zaidi ni kwamba wapinzani wao ligini wamefaulu kugusa nyavu za Man-City mara 22 pekee na hivyo kuwafanya miamba hao kuwa sawa na Liverpool ambao pia wamefungwa mabao machache zaidi (22) hadi kufikia sasa katika EPL msimu huu.