Liverpool na Spurs kujinyanyua UEFA

Liverpool na Spurs kujinyanyua UEFA

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL watakuwa wenyeji wa Rangers leo Jumanne wakilenga kushinda mechi ya pili mfululizo katika Kundi A katika ngarambe ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kufikia sasa, Rangers wanavuta mkia kundini baada ya kupoteza michuano yote miwili ya ufunguzi – Ajax iliwakomoa 4-0 jijini Amsterdam kabla ya Napoli kuwapokeza kichapo cha 3-0 mjini Glasgow.

Hata hivyo, kikosi hicho kinachoshiriki UEFA kwa mara ya kwanza tangu 2010, kinazidi kutamba katika Ligi Kuu ya Scotland na kilitandika Hearts 4-0 ugenini wikendi iliyopita.

Liverpool wanajivunia alama tatu katika Kundi A huku pengo la pointi tatu likitamalaki kati yao na viongozi Napoli watakaowaendea Ajax leo nchini Uholanzi.

Gozi lililoshuhudia Liverpool wakipepeta Ajax 2-1 mwezi uliopita uwanjani Anfield ndilo la pekee ambalo masogora hao wa kocha Jurgen Klopp wameshinda kati ya manne yaliyopita katika mapambano yote.

Sare ya 3-3 dhidi ya Brighton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wikendi iliwasaza miamba hao katika nafasi ya tisa kwa alama 10, sawa na Brentford na Everton. Kikosi hicho kilinyanyua ufalme wa UEFA mnamo 2018-19 kabla ya kutawazwa mabingwa wa EPL msimu uliofuata. Sasa kimeshinda mechi mbili, kupiga sare mara nne na kupoteza mchuano mmoja kati ya saba iliyopita ligini.

Wawakilishi wengine wa Uingereza katika UEFA muhula huu, Tottenham Hotspur, watakuwa na kibarua kigumu cha kujinyanyua leo Jumanne dhidi ya Eintracht Frankfurt katika Kundi D ugenini.

Chini ya kocha Antonio Conte, Spurs walikung’utwa na Arsenal 3-1 katika EPL mnamo Jumamosi huku Frankfurt wakipiga breki kasi ya Union Berlin wanaongoza jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa ushindi wa 2-0 mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Pambano la leo litawapa Frankfurt jukwaa la kushinda mechi yao ya nne mfululizo tangu wacharaze Olympique Marseille 1-0 katika UEFA mnamo Septemba 13 nchini Ufaransa. Kikosi hicho kilifungua kampeni za Kundi D katika UEFA kwa kichapo cha 3-0 kutoka kwa Sporting Lisbon ya Ureno ambayo leo Jumanne itavaana na Marseille ugenini.

Spurs waliweka rekodi ya kuwa kikosi cha kwanza cha Uingereza kupoteza dhidi ya Sporting katika UEFA baada ya kufinywa 2-0 mnamo Septemba 13.

RATIBA YA UEFA (Leo Jumanne):

Bayern vs Viktoria Plzen (7:45pm)

Marseille vs Sporting (7:45pm)

Porto vs Leverkusen (10:00pm)

Club Brugge vs Atletico (10:00pm)

Ajax vs Napoli (10:00pm)

Frankfurt vs Tottenham (10:00pm)

Inter Milan vs Barcelona (10:00pm)

Liverpool vs Rangers (10:00pm)

(Kesho Jumatano):

RB Salzburg vs Dinamo Zagreb (7:45pm)

RB Leipzig vs Celtic (7:45pm)

Chelsea vs AC Milan (10:00pm)

Juventus vs Maccabi Haifa (10:00pm)

Real Madrid vs Shakhtar Donetsk (10:00pm)

Sevilla vs Dortmund (10:00pm)

Benfica vs PSG (10:00pm)

Man-City vs Copenhagen (10:00pm)

  • Tags

You can share this post!

Mashabiki wamtaka Rachier ajiuzulu kwa kukiri ni Freemason

Mung’aro ataja baraza lake la mawaziri

T L