Michezo

Liverpool sasa ina mataji mengi makubwa kuliko Man United

August 15th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Liverpool imepiku mahasimu wao wa tangu jadi Manchester United kwa mataji na sasa ndiyo timu iliyopata ufanisi mkubwa nchini Uingereza baada ya kubeba soka ya Bara Ulaya ya Uefa Super Cup siku ya Jumatano usiku.

Mabingwa wa Klabu Bingwa Ulaya Liverpool, ambao wanafahamika kwa jina la utani kama ‘the Reds’, walichapa washindi wa Ligi ya Uropa Chelsea kwa njia ya penalti 5-4 na kufikisha mataji 46 makubwa.

Mataji ya Liverpool yanajumuisha 18 ya Ligi Kuu, saba ya Kombe la FA, manane ya League Cup, sita ya Klabu Bingwa Ulaya, matatu ya Ligi ya Uropa na manne ya Uefa Super Cup.

Vijana wa Jurgen Klopp waliingia mechi dhidi ya Chelsea wakiwa na mataji 45 makubwa sawa na Manchester United, ambayo inajivunia kushinda ligi mara 20 na mataji 12 ya Kombe la FA, matano ya League Cup, matatu ya Klabu Bingwa Ulaya, moja la Uefa Cup Winners’ Cup, moja ya Ligi ya Uropa, moja ya Uefa Super Cup na moja ya Klabu Bingwa Duniani.

Katika mechi iliyopatia Liverpool taji lake la 46, penalti tisa zilifungwa kabla ya Tammy Abraham kupanguliwa na kipa Adrian.

Mohamed Salah, Trent Alexander-Arnold, Divock Origi, Fabinho na Roberto Firmino walifungia Liverpool nao Jorginho, Ross Barkley, Mason Mount na Emerson wakapachika penalti za Chelsea kabla ya Abraham kupoteza.