Michezo

LIVERPOOL: Taji si lao?

April 25th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MERSYSIDE, Uingereza

MCHANGANUZI wa soka nchini hapa, Rob Smyth amebashiri kwamba Liverpool ina uwezo wa kumaliza Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa jumla ya pointi 97, lakini katika nafasi ya pili nyuma ya Manchester City.

Mdadisi huyo alitoa mfano wa msimu wa 2011-12 ambapo Manchester United walimaliza ligi kwa pointi 89, sawa na Manchester City, lakini wakalikosa taji kutokana na upungufu wa bao moja. Hiyo ilikuwa rekodi ya EPL baada ya misimu 38.

Manchester City na Liverpool zinafukuzana kwa karibu huku msimu ukielekea ukingoni, sawa na ilivyokuwa nchini Italia msimu wa 2017-18 baina ya Napoli na Juventus ambapo mshindi alipatikana siku ya mwisho.

Nchini Uhispania, msimu huo wa 2017-18, kulikuwa na vita vikali kati ya Barcelona na Real Madrid ambapo licha ya kufunga mabao 102 na pointi 92, Madrid chini ya Jose Mourinho walimaliza nyuma ya Barcelona kwa tofauti ya pointi nne pekee.

Lakini hata baada ya kumaliza kwa pointi 96 nyuma ya Barcelona, kocha Manuel Pellgrini alifutwa kazi.

Iwapo Liverpool watamaliza katika nafasi ya pili msimu huu, watakuwa wameweka rekodi ya mara 38, iliyowekwa na klabu ya Celtic iliyopoteza ubingwa kwa Rangers kwa tofauti ya pointi moja tu.

Kabla ya Manchester City kucheza na Manchester United mnamo Jumatano usiku, Liverpool walikuwa uongozini kwa pointi 88 mbele ya Manchester City kwa tofauti ya pointi moja, lakini City walirejea kileleni kwa matokeo ya ushindi.

Mechi tatu

Liverpool wamebakisha mechi tatu mbele ya Huddersfield, Necastle United na mwishowe Wolves.

Baada ya mechi ya Jumatano usiku, Manchester City watakutana na Burnley, Leicester City halafu Brighton.

Man-United ilijiharibia yenyewe kuwa katika mduara wa nne-bora baada ya kupokea kichapo cha 4-0 dhidi ya Everton, kukamilisha mechi tano mfululizo walizopoteza wakiwa katika uwanja wa ugenini baada ya hapo awali kushindwa na Arsenal, Wolves (mara mbili) na miamba wa soka ya Uhispania, Barcelona.

Tangu timu hiyo imwajiri Sir Alex Ferguson mnamo 1986, ilikuwa haijawahi kupoteza mechi tano mfululizo za ugenini ndani ya msimu mmoja.

Kichapo hicho cha mabao mengi zaidi tangu kocha Ole Gunnar Solskjaer apewe kazi ya mkataba wa miaka mitatu, kimekuja wakati timu hiyo imeanza kupata matokeo yasiyoridhisha ambayo yamerudisha kumbukumbu za awali chini ya kocha Jose Mourinho.

Baada ya kuichapa Brighton Jumanne usiku, Spurs wamebakisha kukabiliana na West Ham United, Bournemouth na baadaye Everton.

Spurs, Chelsea na Arsenal zote zimetinga nusu-fainali ya michuano ya kuwania ubingwa wa Ulaya, hapa kukiwa na uwezekano wa timu tano za EPL kufuzu kwa michuano ya UEFA msimu ujao.