Liverpool vs Real Madrid: Leo ni leo!

Liverpool vs Real Madrid: Leo ni leo!

MBIVU na mbichi kuhusu nani ana kiu sana ya kuwa wafalme mpya wa Klabu Bingwa Ulaya kati ya Liverpool na Real Madrid itajulikana watakapofufua uhasama kwenye fainali leo saa nne usiku.

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp, ambayo ina machungu ya kupoteza dhidi ya Real fainali ya 2018, inafukuzia taji la saba baada ya kutawala 1977, 1978, 1981, 1984, 2005 na 2019.

Real imeshinda dimba hilo mara nyingi kuliko wote. Itafikisha mataji 14 ikifanikiwa kuzima Liverpool.

Vijana wa Carlo Ancelotti walitawala kombe hili mara ya mwisho 2018 walipokung’uta Liverpool 3-1 kupitia mabao ya Gareth Bale (mawili) na Karim Benzema jijini Kiev, Ukraine.

Sadio Mane alisawazisha 1-1 dakika chache baada ya Benzema kuweka Real kifua mbele katika mechi hiyo iliyoibua hisia kali kufuatia beki Sergio Ramos kuumiza Salah bega.

Salah alinukuliwa majuzi akisema kuwa ni wakati wa kulipiza kisasi.

Katika kampeni za mwaka huu, mabingwa wa Kombe la FA na League Cup (Carabao) Liverpool walibandua Inter Milan, Benfica na Villarreal katika raundi tatu zilizopita.

Nao Real walikanyaga Paris Saint-Germain, Chelsea na Manchester City mtawalia.Mabingwa wa LaLiga, Real, wana rekodi nzuri dhidi ya Liverpool.

Baada ya kupepetwa mara tatu mfululizo kati ya 1981 na 2009, Real wamelemea Liverpool mara nne na kutoka sare tasa walipokutana mara ya mwisho katika mechi ya marudiano ya robo-fainali ya 2020-2021.

Liverpool ilipoteza mara ya mwisho katika mashindano yote mnamo Machi 8 ilipopigwa na Inter Milan 1-0 ugani Anfield. Tangu wakati huo, haijapoteza michuano 18, ikizoa ushindi mara 10 katika mechi 11 zilizopita.

Katika idadi sawa ya mechi, Real imeshinda 12 ikatoka sare mara mbili na kulemewa mara nne. Ilitoka sare dhidi ya Cadiz na Real Betis katika michuano miwili iliyopita ligini. Macho yatakuwa kwa washambulizi Salah na Benzema walioibuka wafungaji bora katika ligi zao msimu huu uliokamilika wikendi jana, kwa mabao 23 na 27 mtawalia.

Habari za kutia moyo kambini mwa Liverpool ni kuwa kiungo Fabinho amerejea baada ya kupona jeraha la paja alilopata dhidi ya Aston Villa mwanzoni mwa mwezi huu. Alikosa mechi dhidi ya Southampton na Wolves. Naye beki Joe Gomez alikuwa mkekani dhidi ya Wolves akiuguza jeraha la kifundo, lakini Liverpool ina imani atakuwa sawa dhidi ya Real.

Kuna hofu pia kuhusu kiungo Thiago Alcantara aliyekuwa na tatizo la kisigino, lakini Klopp ana matumaini kuwa anaweza kushiriki mchuano wa kesho. Mshambulizi Divock Origi yuko nje na tatizo la msuli. Hakuna ripoti ya majeruhi kambini mwa Real.

Mshindi atatuzwa donge nono la Sh2.6 bilioni pamoja na tiketi ya kuvaana na mabingwa wa kombe toto la Europa League, Eintracht Frankfurt, katika kipute cha Uefa Super Cup mwezi Agosti.

Pia ushindi leo Jumamosi ni tikiti ya kushiriki makala yajayo ya Klabu Bingwa Duniani (Club World Cup). Naye nambari mbili hii leo atatia mfukoni Sh2.0 bilioni.

  • Tags

You can share this post!

Tutanasa magari yote ya serikali, Chebukati aonya wagombea

Jinsi wanaume wanavyoporwa mali kwa ahadi za ngono

T L