Liverpool waafikiana na RB Leipzig kumsajili beki Konate kwa Sh4.8 bilioni mwisho wa msimu huu

Liverpool waafikiana na RB Leipzig kumsajili beki Konate kwa Sh4.8 bilioni mwisho wa msimu huu

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL wameafikiana na kikosi cha RB Leipzig nchini Ujerumani kwamba watamsajili beki raia wa Ufaransa, Ibrahima Konate, 21, kwa kima cha Sh4.8 bilioni mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Habari hizo ni pigo kwa Manchester United waliokuwa wakimvizia pia mwanasoka huyo ambaye kwa sasa atahudumu uwanjani Anfield kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Liverpool walilazimika kufanya usajili wa haraka mnamo Januari 2021 na wakajinasia huduma za mabeki Ozan Kabak na Ben Davies baada ya safu yao ya ulinzi kulemewa na wingi wa visa vya majeraha.

Hata hivyo, Konate ni suluhu ya kudumu kwa matatizo ambayo Liverpool wameshuhudia kwenye idara yao ya nyuma msimu huu, huku akitarajiwa kushirikiana vilivyo na madifenda Joel Matip, Joe Gomez na Virgil van Dijk kuanzia msimu wa 2021-22.

Licha ya majeraha ya mara kwa mara kumtatiza msimu huu, Konate ambaye ni tegemeo kubwa katika timu ya taifa ya Under-21 nchini Ufaransa, aliwaongoza Leipzig kupiga hatua kwenye soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Jeraha la misuli lilimfanya Konate kuwajibishwa na Leipzig mara nane pekee katika msimu wa 2019-20 huku tatizo la kifundo cha mguu likimweka nje ya michuano mingi ya muhula huu.

Kufikia sasa, sogora huyo amechezeshwa na Leipzig mara 12 katika kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga). Baada ya kujihakikishia saini ya Konate, Liverpool kwa sasa wanatarajiwa kuimarisha juhudi zao za kusajili wanasoka Memphis Depay na Sander Berge kutoka Olympique Lyon na Sheffield United mtawalia.

Liverpool wangali katika vita vya kupigania fursa ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa nne-bora msimu huu na kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Ni matarajio ya kocha Jurgen Klopp kwamba usimamizi utapiga jeki juhudi zake za kukisuka upya kikosi chake ambacho anaamini kitatawaliwa na kiu ya kujinyanyulia mataji mengi msimu ujao wa 2021-22.

Kufikia sasa, Liverpool wameordhesha wanasoka watano wanaolenga kusajili mwishoni mwa msimu huu ili kujiweka sasa kwa kampeni za muhula ujao.

Liverpool pia wamefichua mpango wa kumpa Kabak, 21, mkataba wa kudumu baada ya kipindi cha mkopo wa sogora huyo raia wa Uturuki aliyesajiliwa kutoka Schalke ya Ujerumani mnamo Januari 2021 kutamatika rasmi.

Iwapo watashawishika kufanya hivyo, basi mabingwa hao watetezi wa EPL watalazimika kuweka mezani kima cha Sh2.5 bilioni kwa minajili ya Kabak.

Kufikia sasa, Kabak amechezeshwa na Liverpool mara nane ligini na akawa sehemu ya michuano yote ya mikondo miwili iliyoshuhudia Liverpool wakidengua Leipzig kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu.

Konate alisalia benchi wakati wa mechi zote mbili zilizoshuhudia Liverpool wakifunga Leipzig jumla ya mabao 4-0.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ana matumaini tele kushiriki katika raga ya hadhi akifuata...

Ngara Sportiff kujikaza kiume kumaliza kileleni