Michezo

Liverpool waangusha Leicester na kuweka rekodi mpya ya kutoshindwa ugani Anfield

November 23rd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL sasa wanajivunia alama sawa na Tottenham Hotspur kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupepeta Leicester City 3-0 mnamo Novemba 22, 2020 ugani Anfield.

Japo wameorodheshwa nyuma ya Spurs kutokana na uchache wa mabao, ushindi mnono uliosajiliwa na masogora hao wa kocha Jurgen Klopp ni onyo kubwa kwa washindani wengine wanaowania fursa ya kuwapokonya Liverpool ubingwa wa taji la EPL msimu huu.

Kwa kuzamisha chombo cha Leicester, Liverpool waliweka rekodi mpya ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 64 zilizopita za ligi ugani Anfield. Mabingwa hao watetezi wa EPL walivunja rekodi yao ya awali iliyowashuhudia wakipiga msururu wa mechi 63 za ligi bila ya kupoteza hata moja kati ya Februari 1978 na Januari 1981. Leicester ndio waliopiga breki rekodi hiyo ya Liverpool wakati huo.

Kubwa zaidi linalostahili kuwa kiini cha matumaini kwa mashabiki wa Liverpool kwamba kikosi chao kina uwezo wa kuhifadhi ufalme wa EPL msimu huu ni kwamba walizamisha chombo cha Leicester bila ya kujivunia huduma za baadhi ya wanasoka wao mahiri.

Miongoni mwa wachezaji hao matata waliokosa kuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Klopp dhidi ya Leicester ni Virgil van Dijk, Trent Alexander-Arnold, Joe Gomez, Jordan Henderson, Thiago Alcantara na Mohamed Salah.

“Kulikuwa na mambo mengi mazuri katika mechi hiyo. Siwezi nikateua moja lililonifurahisha zaidi. Pengine matokeo ya kuridhisha zaidi kutoka kwa James Milner aliyechezeshwa kama beki wa kulia,” akatanguliza Klopp.

“Alijituma zaidi katika nafasi hiyo kabla ya kuendeleza ubabe wake alipoenda kwenye safu ya kati. Hilo ndilo tunalotarajia kutoka kwa kila mmoja wetu.”

“Majeraha yalikuwa mengi na yalitushangaza sote. Lakini iliwalazimu vijana wenyewe kutafuta suluhu. Tuna idadi kubwa ya mabeki chipukizi ambao pia wanaweza kuwajibishwa kama viungo wakabaji. Japo hawana tajriba pevu, walipania kujituma kadri ya uwezo wao,” akaongeza kocha huyo raia wa Ujerumani.

Liverpool walijipata uongozini kunako dakika ya 21 kupitia kwa Jonny Evans aliyejifunga kabla ya sajili mpya Diogo Jota kuongeza bao la pili dakika nne kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa. Bao la Jota ambaye ni mchezaji wa zamani wa Wolves, lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na beki Andrew Robertson.

Kukosekana kwa Salah kulimpa Jota fursa ya kuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Liverpool kuwahi kufunga katika mechi nne za kwanza ugani Anfield.

Baada ya kufungiwa bao la tatu na Roberto Firmino katika dakika ya 86, Liverpool walipoteza fursa mbili za kupachika wavuni magoli mawili zaidi kupitia kwa fowadi Sadio Mane aliyemtatiza pakubwa kipa Kasper Schmeichel.

Chini ya kocha Brendan Rodgers, Leicester waliingia ugani wakipigiwa upatu wa kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakipokeza Manchester City kichapo cha 5-2 kabla ya kuzamisha chombo cha Arsenal na Leeds United.

“Tulifunga mabao matatu na wapinzani hawakutikisa nyavu zetu. Tulidhibiti mechi na kuimakinikia safu ya ulinzi vilivyo,” akasema Klopp kwa kuwataka chipukizi wake kujituma hata zaidi na kujipa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza hasa ikizingatiwa kwamba kiungo Naby Keita naye alipata jeraha katika mechi hiyo.

Kati ya mechi 64 ambazo Liverpool hawajapoteza nyumbani, miamba hao wamesajili ushindi mara 53.

Tangu Rodgers apokezwe mikoba ya Leicester, kocha huyo ameshuhudia kikosi chake kikipoteza mechi tatu za EPL mikononi mwa Liverpool ambao wamewafunga jumla ya mabao tisa.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kuwa wenyeji wa Atalanta kutoka Italia katika gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 25, 2020 kabla ya kuwaendea Brighton kwa mechi ya EPL mnamo Novemba 28.

Kwa upande wao, Leicester wameratibiwa kuchuana na Braga ya Ureno katika mechi ya Europa League mnamo Novemba 26 kabla ya kuwaalika Fulham kwa mchuano wa EPL uwanjani King Power mnamo Novemba 30, 2020.