Liverpool wadhalilisha Man-United kwenye EPL ugani Old Trafford

Liverpool wadhalilisha Man-United kwenye EPL ugani Old Trafford

Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United amesema hawezi kutamauka sasa katika safari ya kudhibiti mikoba ya waajiri wake kwa sababu “ametoka nao mbali sana”.

Hii ni licha ya kikosi chake kinachojivunia kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mara 20 kupokezwa kichapo cha 5-0 kutoka kwa Liverpool katika kipute hicho mnamo Jumapili uwanjani Old Trafford.

Mohamed Salah alifungia Liverpool mabao matatu huku mengine yakipachikwa wavuni kupitia Naby  Keita na Diogo Jota.Solskjaer ambaye ni raia wa Norway, alisema ingawa siku ya kichapo hicho “ndiyo mbaya zaidi” katika historia yake ya ukufunzi, bado ataendelea kuhudumu uwanjani Old Trafford.

“Najua kwa sasa tuko katika ubovu wetu na sidhani kuna jinsi yoyote ya kuelezea masikitiko yetu. Tutaona mahali kichapo hiki kitatuweka,” akatanguliza Solskjaer katika mahojiano yake na Sky Sports. “Nimetoka mbali na tumetoka mbali kama kundi. Tuko karibu sana kuwa thabiti na hatuwezi kukata tamaa kwa sasa,” akasema.

Alipoulizwa kuhusu jinsi anavyopanga kuwanyanyua masogora wake na kuwasaidia kuweka kando maruerue ya kichapo hicho, Solskjaer aliongeza: “Itakuwa vigumu. Bila shaka wachezaji wamejihisi vibaya na motisha yao imeshuka. Lakini pia tuna wachezaji walio na uthabiti mkubwa kiakili ambao watajitoa topeni upesi,” akaeleza.

Ushindi huo ulikuwa mnono zaidi kuwahi kusajiliwa na Liverpool katika historia yao uwanjani Old Trafford. Kwa upande wa Man-United, hicho kilikuwa kichapo kinono zaidi kwa Liverpool kuwahi kuwapokeza tangu Oktoba 1895 ambapo walipigwa 7-1 uwanjani Anfield.

Aidha, ilikuwa mara yao ya kwanza tangu 1955 kupoteza mechi kwa mabao matano au zaidi ugani Old Trafford bila ya wao wenyeji kufunga. Mashabiki wa Man-United waliondoka uwanjani mwishoni mwa kipindi cha kwanza matokeo yalipokuwa 4-0 japo timu yao ilifungwa mara moja pekee katika kipindi cha pili baada ya kiungo Paul Pogba kuondolewa kwa kadi nyekundu dakika 15 pekee baada ya kuletwa uwanjani katika kipindi cha pili.

“Si rahisi kusema chochote isipokuwa kusisitiza kwamba hii ndiyo siku mbovu zaidi nimewahi kuona nikidhibiti mikoba ya Man-United,” akaongeza Solskjaer aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Jose Mourinho mnamo 2018.

“Hatukucheza vizuri kama timu na katika kiwango cha mtu binafsi. Tulitepetea mno na kusuasua katika kila idara na Liverpool wakapata fursa ya kutudhalilisha,” akasema beki na nahodha wa Man-United, Harry Maguire aliyeomba radhi kutoka kwa mashabiki kwa sababu ya matokeo duni kutoka kwao.

You can share this post!

TAHARIRI: Vurugu za kisiasa ni aibu, zikabiliwe

Tielemans na Maddison wasaidia Leicester kuzamisha chombo...

T L